Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Ilela wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuishi porini wakiwa katika makazi yao mapya kama wanavyoonekana pichani. |
Na Muhidin
Amri,
Mbinga.
ZAIDI ya watu 200 waishio katika kijiji cha Ilela kata ya
Mikalanga wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamehama makazi yao na kulazimika
kuishi porini kwa kile walichoeleza kuwa wanaepuka kukamatwa, kuwekwa mahabusu
na kuteswa na askari Polisi wa kituo kidogo cha Maguu wilayani humo ambao
wanalazimisha kutoa michango ya fedha, kwa ajili ya ujenzi wa kituo kidogo cha
polisi katika kata hiyo.
Mbali na hilo watoto chini ya miaka mitano wanashindwa kupata
huduma ya matibabu ya kliniki, baada ya uongozi wa kijiji hicho kudaiwa
kuandika barua kwenda uongozi wa zahanati ya Ilela ikizuia watoto wenye wazazi
ambao wamekimbilia porini, wasipatiwe huduma ya matibabu.
Akina mama nao imefikia hatua sasa, hulazimika kutembea
umbali wa kilometa tisa kwenda katika kijiji cha Burma, kufuata huduma hiyo ya matibabu
kwa watoto wao.
Kufuatia hali hiyo, pia wanamtuhumu Diwani wao wa kata hiyo Joachimu
Kowelo kwa kitendo chake cha kuwagawa wananchi wa kata hiyo kwa kuuagiza
uongozi wa kijiji na kata kuwahamisha kwa nguvu baadhi ya wananchi wake,
wakaishi kijiji kipya cha Ugogo kwa maslahi yake binafsi kitendo ambacho kimefafanuliwa
kuwa ni cha kinyama.
Wakazi hao waliendelea kueleza kuwa, wamelazimika kuhama
katika nyumba zao na kukimbilia kuishi porini kwa lengo la kuepuka manyanyaso
wanayoyapata kutoka kwa askari hao Polisi wa kituo cha Maguu, ambao huvamia
makazi yao nyakati za usiku na kulazimisha wananchi watoe michango.
Walieleza kuwa kila siku wamekuwa wakiishi kwa taabu, huku
wakikesha usiku kucha kuwakimbia askari hao ambao hufika nyakati za usiku
wakiwakamata na kuwaweka mahabusu, na kuwatoza shilingi 45,000 kama dhamana na
shilingi 87,000 kwa ajili ya uendeshaji wa kazi za polisi jambo ambalo ni la
uonevu na la kusikitisha.
Kwa mujibu wa maelezo ya wakazi hao wameendelea kumnyoshea
kidole Diwani wao Kowelo, wakisema ndio chanzo cha hayo matatizo wakidai kuwa
ameapa kuwashughulikia watu wote wanaompinga katika harakati za kutaka kurudi
tena madarakani katika kugombea, kwenye nafasi hiyo ya udiwani.
Veronica Mbele, Edwin Nombo, Suzy Mahayi na Menas Nombo
walisema kwa nyakati tofauti diwani wao ndiye aliyeshinikiza kwa uongozi wa
kijiji na kata ili wahamie katika kijiji cha Ugogo na kuwatumia askari hao
wawaletee usumbufu, ikiwemo kuwafungulia hata mashtaka ambayo hayana ukweli
huku wengine wakiapa kwamba wapo tayari kufia katika kijiji cha Ilela, na sio
huko ambako wanalazimishwa wahamie.
Walisema wao wanahitaji kuendelea kuishi katika kijiji hicho,
kwani hakuna sababu ya msingi ya wao kupelekwa huko licha ya serikali kukigawa
kijiji cha Ilela na kuzaliwa kijiji cha Ugogo, huku wakiongeza kuwa hawana
ulazima wao kwenda kijiji hicho kipya kwani tayari wana makazi ya kudumu katika
kijiji cha Ilela na ambako wanapata huduma za maji na tiba.
Angelus Komba, naye alisema licha ya kijiji cha Ugogo kuundwa
kisheria hakuna sababu ya kulazimisha watu wakaishi huko, badala yake ni vyema
ukafanyika utaratibu wa kukaa na wananchi husika kwa kufanya kikao cha pamoja
cha maradhiano, jambo ambalo halijafanyika hadi sasa badala yake diwani ndiye
anayeonekana kufanya mambo hayo ya kipuuzi ya kutesa wapiga kura wake, hasa kwa
mtu ambaye anampinga katika shughuli zake za kiutawala.
Diwani wa kata ya Mikalanga, Joachimu Kowelo alikana kuhusika
na tuhuma hizo ambapo alieleza kwamba wananchi hao hawakupaswa kuyakimbia
makazi yao.
“Hawa wananchi ni wapuuzi sana, mimi binafsi nashindwa kuwaelewa
ni sababu gani ya msingi iliyowafanya wayakimbie makazi yao na kwenda kuishi
porini, hizi najua ni njama za kisiasa tu”, alisema Kowelo.
Hata hivyo jitihada ya kumpata Kamanda wa polisi wa mkoa wa
Ruvuma, Mihayo Msikhela ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya tuhuma
wanazotuhumiwa askari wake ziligonga mwamba na simu yake, ilikuwa ikiita kwa
muda mrefu bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment