Cresencia
Kapinga,
Songea.
NAIBU katibu Mkuu bara, Chama Cha Wananchi (CUF) Magdalena
Sakaya amewataka wananchi wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, wafanye
mabadiliko kwa kutokipatia kura ya ndiyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi
mkuu ujao, kwa kile alichodai kuwa chama hicho kimekuwa kikiwacharaza bakora za
ugumu wa maisha na kuwafanya vijana wazeeke kabla ya wakati wao.
Akihutubia kwenye mkutano wa chama hicho ambao ulifanyika
katika viwanja vya Majengo mjini hapa, Magdalena alikirushia kombora CCM
akisema kuwa ndio kilichowafikishia wananchi wake ugumu wa maisha waliyonayo sasa watanzania, na kusababisha migogoro na migomo ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Naibu katibu huyo alieleza kuwa hata gharama za maisha hivi
sasa zimepanda tofauti na miaka ya nyuma, jambo ambalo mwananchi mwenye kipato
cha chini huendelea kuwa masikini na kuteseka na maisha.
“Nikiangalia hapa vijana wengi wa Songea nyuso zenu ni za hazuni tupu, hii inatokana na ugumu wa maisha ambayo yameletwa na chama hiki tawala
vijana wengi wamekuwa wazurulaji, wazee hawapati matibabu bure hali kadhalika
akina mama wanapokwenda kujifungua hospitali wanapata taabu tu”, alisema
Sakaya.
Alifafanua kuwa wakati umefika kwa wakazi wa Songea kufanya
mabadiliko na kuachana na sera za Chama cha mapinduzi, kwani mikoa yenye
viongozi kutoka vyama pinzani imekuwa na maendeleo makubwa kutokana na CCM imekuwa
ikiwahonga wananchi kwa kuwapelekea maendeleo haraka ili waichague.
“Mji wa Songea ni mji mkongwe, lakini miundombinu yenu ni
mibovu hata umeme imekuwa ni tatizo upatikanaji wake, maji hakuna na hata
huduma za afya imekuwa ni tatizo lazima niwaambie ukweli ndugu zangu, kwa
sababu CCM inawafanya nyie kama tenga la kuku ambao mkipewa mahindi mnakula,
mchele mnakula wakati umefika sasa wa kufanya mabadiliko ya kweli ili tuweze
kuondokana na karaha hizi”, alisema.
Vilevile amewataka wananchi wa Songea watambue kuwa chama
hicho tawala, kinawadanganya wananchi wake kama wanavyofanya wauzaji wa pombe
haramu aina ya gongo, ambapo wanabadilisha chupa lakini gongo ni ile ile.
Kadhalika amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kujitokeza
kwa wingi na kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili kila
mmoja aweze kwenda kupiga kura muda wa uchaguzi utakapowadia na kwamba endapo
hawatatimiza hilo watakuwa wamekosa haki yao ya msingi, ya kupiga kura au
kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Hata hivyo akiwa katika mkoa huo Naibu katibu Mkuu wa CUF,
Sakaya ameweza kufanya mikutano yake katika kata ya Madaba, Songea vijijini na
Majengo iliyopo Manispaa ya Songea ambapo ziara yake inaendelea katika wilaya
ya Namtumbo na kumalizia wilaya ya Tunduru.
No comments:
Post a Comment