Na Muhidin
Amri,
Namtumbo.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma, Stephen Nana amewataka Madiwani wa halmashauri hiyo kujifunga kibwebwe
katika kusimamia mapato sambamba na ukusanyaji wa ushuru ipasavyo, ili kuifanya
wilaya hiyo iweze kusonga mbele kimaendeleo.
Nana alitoa rai hiyo juzi, alipokuwa akifungua kikao cha robo
mwaka cha baraza la madiwani hao huku akisisitiza muda wa kufanya kazi kwa
mazoea umepita kilichobaki sasa ni kuhakikisha wananchi, wanapatiwa huduma za
kijamii kwa wakati.
Alifafanua kuwa muda uliobaki kabla ya kufanyika uchaguzi
mkuu ujao, ni vizuri kila diwani ajitathimini mwenyewe, namna alivyoleta mchango
wa maendeleo kwa wananchi wake na wilaya kwa ujumla.
Kadhalika aliwataka kusimamia na kutekeleza maamuzi yote
yanayofikiwa katika vikao husika, na kuacha tabia ya kuwa vigeu geu kwani
kufanya hivyo kunaweza kurudisha nyuma mipango mbalimbali, inayofikiwa katika
vikao hivyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, baadhi ya
Madiwani kutokana na kuwepo na tabia ya kujenga maslahi yao binafsi wamekuwa
wakipindisha kwa makusudi sheria na kanuni zilizopo, kwa lengo la kujinufaisha
wao wenyewe na kuiacha jamii ikiendelea kuteseka.
“Madiwani wenzangu ni lazima sasa tubadilike, hatutakiwi kuwa
vigeu geu sisi ni watu wazima wananchi walituamini na kutuweka madarakani ni
vizuri sasa safari hii tuliyoianza mwaka 2010, tuimalize tukiwa salama bila
kuwepo malalamiko ya hapa na pale”, alisema Nana.
Pamoja na mambo mengine, watumishi wa Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo aliwataka kuacha tabia ya kulala usingizi sehemu ya kazi badala
yake wajitume ili kuweza kuongeza ufanisi katika kazi zao za kila siku, ili
kuondoa umasikini uliokithiri katika wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment