Kassian Nyandindi |
Na Kassian Nyandindi, Uchambuzi.
TATIZO la upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mji
wa Mbinga, hivi sasa imekuwa ni kero kiasi ambacho wakazi wa mji huo wameanza
kulalamikia hali hiyo.
Binafsi nimelichunguza tatizo hili na kubaini TANESCO kuanzia ngazi ya wilaya hadi huko juu,
ni muhimu kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili isiweze kuendelea na
kuleta malalamiko yasiyo ya lazima miongoni mwa jamii.
Ukosefu wa umeme wa uhakika katika mji huu wa Mbinga
unatokana na Transfoma yenye ukubwa wa KVA 100 – 11KV kushindwa kufanya kazi
yake ipasavyo kwa sababu ya kubebeshwa mzigo mkubwa nje ya uwezo wake.
Transfoma hiyo ndio kiini kikuu ambacho hutegemewa
kusambaza nishati hiyo muhimu katika maeneo ya viwanda, mashine za kukobolea
nafaka na maeneo mengine ya nyumba za kuishi watu.
Ninachoweza kuuliza hapa ni kwamba TANESCO Mbinga
mlikuwa mkifanya nini siku zote hizi hadi Transfoma hii inazidiwa katika
kufanya kazi yake, ukizingatia kwamba wateja Mbinga sasa wanaongezeka kila
kukicha.
Huu ni uzembe, kwa sababu binafsi natambua mlikuwa
mkijua kwamba kadiri wateja mnavyozidi kuwaunganishia “Service line” walikuwa
wakiongezeka, sasa mlikuwa wapi kutafuta Transfoma nyingine ya akiba ili
kunusuru hali hii isiweze kutokea?
Katika maeneo ya viwanda na mashine ya kukobolea
nafaka hapa Mbinga mjini, tunakosa huduma husika kutoka katika maeneo hayo na
kutufanya shughuli zetu za kimaendeleo zishindwe kutekelezwa ipasavyo, yatupasa
tuelekeze lawama zetu kwenu.
Lawama hizi apelekewe nani kama sio ninyi, ambao
mmeshika hatamu ya kuongoza na kusimamia shirika hilo la ugavi wa umeme hapa
Mbinga.
Hivi sasa umeme unaosambazwa katika mji huu sio wa
uhakika hivyo, ofisi ya TANESCO ifanye mawasiliano na ofisi husika ili tuweze
kuletewa transfoma nyingine haraka, kwa ajili ya kuongeza nguvu ya usambazaji
wa nishati hiyo.
Nakumbuka majira ya saa nane mchana Desemba 31 mwaka
jana, ndipo tatizo hili lilianza kujitokeza baada ya wateja wenu kuwapigia simu
kuwa transfoma iliyopo eneo la ofisi za idara ya ujenzi inatoa moshi na mlipoichunguza
mlibaini kuwa imezidiwa, sasa tunahitaji utekelezaji wa haraka ili tuondokane
na kero hii.
Hata hivyo Meneja wa shirika hilo la ugavi wa umeme
hapa Mbinga Kanut Punguti, nimemnukuu akisema kasi ya upatikanaji wa transfoma
nyingine itategemea na mchakato utakaofanywa na uongozi wa shirika hilo ngazi
ya mkoa.
Nasema kauli hii inakatisha tamaa, na inaonesha
upatikanaji wa chombo hiki utachelewa na wala tusitegemee kupata haraka, je
tutafika kweli?
Ni vyema sasa uongozi wa Taifa makao makuu ya TANESCO,
waingilie kati suala hili, ili wanambinga tuweze kupata umeme wa uhakika kama
ilivyokuwa awali, hatuhitaji kupewa kauli ambazo utekelezaji wake unaonesha kwenda polepole.
No comments:
Post a Comment