Na Kassian Nyandindi,Mbinga.
ALIYEKUWA mkuu wa wilaya ya Makete, Osmund Kapinga amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akituhumiwa kuiba shilingi milioni 26 mali ya kampuni ya Songea Network Solution iliyopo mjini hapa.
Mwendesha mashtaka wa polisi sajenti Seif alidai mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya hiyo Joackimu Mwakyolo, kuwa mkuu wa wilaya mstaafu Osmund Kapinga aliiba fedha hizo.
Seif aliendelea kudai mahakamani hapo kwamba, Kapinga alitenda kosa hilo kwa kushirikiana na mdogo wake aliyetajwa kwa jina la John Kapinga ambapo waliiba fedha hizo ambazo ilitakiwa wazitumie kununulia kahawa vijijini kwa wakulima wilayani Mbinga.
Alidai kuwa mnamo Septemba 2 na Oktoba 25 katika msimu wa manunuzi ya zao hilo mwaka jana, walichukua shilingi milioni 19 kwa lengo la kwenda kununua kahawa lakini hawakufanya hivyo hadi mwisho wa msimu.
Aidha katika hatua nyingine ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao katika kipindi hicho walikwenda katika kijiji cha Lunoro ambapo walikutana na kikundi cha uzalishaji wa kahawa cha Nuntura, na kuchukua kahawa yenye thamani ya shilingi milioni 7 huku wakulima wa kikundi hicho wakiendelea kudai malipo yao hadi leo hii.
Seif alidai kuwa fedha za malipo ya kahawa hiyo zilikwisha tolewa na kampuni ya Songea Network Solution na kukabidhiwa watuhumiwa hao ili wakawalipe wakulima, lakini hawakufanya hivyo.
Hata hivyo washtakiwa hao wote kwa pamoja wamekana mashtaka na wapo nje kwa dhamana, hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Februari 14 mwaka huu.
.
No comments:
Post a Comment