Monday, January 14, 2013

WALEMAVU MBINGA WAPATIWA MAFUNZO YA KUANZISHA NA KUENDESHA BIASHARA KWA MAFANIKIO PAMOJA NA MPANGO MKAKATI

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tano yanayohusu Kuanzisha na kuendesha biashara kwa mafanikio pamoja na mpango mkakati, wakifuatilia leo kwa umakini mada ambazo zilikuwa zikitolewa na mkufunzi wa kutoka Chemba ya wafanyabiashara na wenye viwanda(TCCIA) tawi la wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, Philomen Msigwa, (hayupo pichani). Walioshiriki mafunzo hayo ni walemavu wa makundi mbalimbali wanaoishi wilayani humo.(Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

 

JAMII imetakiwa kuondokana na dhana potofu ambayo imejengeka miongoni mwao kwamba, watu walio katika kundi lenye ulemavu ni mzigo na hawezi kufanya shughuli za kimaendeleo katika jamii.


Kauli hiyo ilitolewa leo na ofisa mtendaji wa Chemba ya wafanyabiashara na wenye viwanda(TCCIA) tawi la wilaya ya Mbinga, Philomen Msigwa kwenye ukumbi wa UVIKITWE uliopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, katika mafunzo ya siku tano ya kuwawezesha baadhi ya walemavu wa wilaya hiyo kuanzisha na kuendesha biashara kwa mafanikio kwa kuzingatia mpango mkakati.


Msigwa alisema jamii inafanya makosa kuwadharau watu wenye hali hiyo, huku wengine wakifikia hatua ya hata kuwaficha ndani ya majumba yao.


Alisema kufanya hivyo kunahatarisha ustawi wa maendeleo ya watu hao na taifa kwa ujumla, hivyo ni jukumu sasa la serikali na jamii inayowazunguka kuona kwamba kundi hilo linashiriki kikamilifu katika kuwapa fursa ambazo zitawafanya wasiwe tegemezi.


Akizungumzia juu ya mafunzo hayo alisema wakati huu ni wa soko huria na utandawazi hivyo watu binafsi au kundi fulani, linaruhusiwa kufanya biashara yeyote kwa kufuata misingi halali iliyowekwa na serikali.

 

"Kumekuwa na msukumo mkubwa kutoka serikalini na mashirika ya kimataifa, kuwahimiza watu kuanzisha biashara au miradi mikubwa na midogo, hivyo jamii inatakiwa ishiriki kikamilifu katika hili", alisema.


Vilevile alieleza kuwa hali zinazohitaji uangalifu katika kutaka kufanikiwa kijasiriamali ni muhimu kukamilisha matakwa yote ya kisheria, lenga biashara halali ya kufanya na kufanya biashara ambazo hazina athari kwa mazingira au jamii.

 

Pia Msigwa aliwafundisha walemavu hao namna ya kupata wazo zuri la biashara au mradi, na namna ya kufanya biashara hiyo kwa malengo yakinifu na yenye tija.


Mafunzo hayo yamefadhiliwa na shirika la "The foundation for civil society" la kutoka Jijini Dar es Salaam, yakilenga hasa walemavu hao kufundishwa juu ya dhana inayohusu mpango mkakati.

 

 

 


 

No comments: