Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAZAZI na walezi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameaswa kushirikiana na serikali kusimamia na
kufuatilia kwa karibu mienendo na maendeleo ya watoto wao hasa wa
kike, ikiwa ni juhudi ya kuhakikisha kuwa watoto hao
wanafanya vizuri katika masomo yao na kujiletea maendeleo yao.
Ofisa mtendaji wa kata ya Muhuwesi Shijabu Ngoronje alisema hayo wakati alipokuwa
akizungumza kwenye mkutano wa Wadau wa elimu uliofanyika katika Kijiji cha
Mhuwesi, ukiwa ni mwendelezo wa juhudi za mradi wa usimamizi na utetezi
wa haki ya mtoto wa kike kupata elimu .
Akifafanua taarifa hiyo Ngoronje alisema, ili kufanikisha adhima hiyo
serikali imejipanga kutoa elimu kwa kuwaomba wazazi na walezi kujitoa kuchangia
chakula cha mchana kama kivutio kwa watoto wao na kuwafanya wapende
masomo.
Kuhusu mila na desturi za makabila ya Wayao wilayani Tunduru, alisema
kuwa tayari serikali imeunda kikosi kazi cha kuonana na viongozi wa mila,
makungwi na manyakanga na kuwaomba wasaidie kuiwaelimisha juu ya utoaji wa
elimu kwa watoto wa kike, na kuwafanya wapende masomo tofauti na sasa ambapo
kundi hilo limekuwa likifundishwa kukabiliana na maisha ya ndoa hali inayosababisha
kuwepo kwa matukio mengi ya ndoa za utotoni wakiwa shuleni.
Kuhusu wazazi wenye tabia za kutunza siri za watoto wao wakike baada ya
kupewa mimba na wanaume kwa kisingizio cha kutaka kuwaozesha mapema
alisema , serikali imejipanga kupambana nao kwa kuanza kuwachukulia hatua
wazazi na watoto husika pamoja na manyakanga ambao wamekuwa wakitoa mafunzo
mabaya wakati wa jando na unyago.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Hakimu
Kilowa na Hussein Makoroboyi katika maoni yao juu ya kinacho
sababisha elimu kushuka wilayani humo, walidai kuwa Kipato duni cha akina mama ndio
chanzo kikuu, ambapo mara nyingi ndio wamekuwa wakiachiwa jukumu la kutunza watoto
wa kike .
Aidha wadau hao
pia wakatumia nafasi hiyo kuwashukuru kuwapongeza wafadhili wa mradi huo Shirika la The Foundation
for Civil Society (FCS) la Jijini Dar Es Salaam, kwamba mradi huo utaweza kuongeza msukumo kwa wazazi kuwahimiza
watoto wao kwenda shule, pia kuwa apunguzia majukumu watoto wa kike na kuwaoza
mapema kabla ya umri wao.
Shekh mkuu wa Tunduru
Alhaji Waziri Chilakwechi alipongeza kuwepo kwa mradi huo, ambao alisema
kuwa ni ukombozi kwa mtoto wa kike na utaweza kuongeza msukumo kwa wazazi
kuwahimiza watoto wao kwenda shule, pia kuwapunguzia majukumu watoto wa kike na
kuwaoza mapema kabla ya umri wao.
Awali akitoa taarifa ya maradi huo Meneja wa mradi wa shirika
kiserikali la TUFAE Education Aids Trust, linalo simamia uhamasishaji huo John
Nginga alisema kuwa mradi huo ulibuniwa kufuatia majibu mabaya ya utafiti
uliofanywa na shirika hilo mwaka 2007 hadi 2010 na kubaini uwepo wa maendeleo
mabaya ya elimu kwa mtoto wa kike wilayani humo, na kuchukua uamuzi wa
kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anapata elimu kuanzia darasa la awali,
elimu ya msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu.
Bw.
Nginga aliendelea kubainisha kuwa katika utafiti huo uliofanyika katika tarafa
za Muhuwesi, Namasakata, Ligoma, Nandembo, Mlingoti Mashariki na Mlingoti
Magharibi wilayanbi Tunduru zilibainisha kuwapo kwa kundi kubwa la watoto wa
kike waliopata mimba pamoja na kikwazo cha uelewa mdogo wa jamii juu ya sera ya
elimu, haki ya mtoto wa kike kupata elimu na mila zilizopitwa na wakati.Takwimu hizo zilifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2007hadi 2010 jumla ya waliotarajiwa kuandikishwa shule ni watoto wa kike 17,386, walioandikishwa ni 14,692 ambao ni sawa na asilimia 85.49% na waliosajiliwa ni 13,411, na waliofanya mitihani wa kumaliza darasa la saba walikuwa 13,097 ambao ni sawa na asilimia 97.65%, huku kukiwa na anguko la watoto 314 ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata mimba wakiwa shuleni pamoja na utoro.
No comments:
Post a Comment