Thursday, January 17, 2013

WAKULIMA WA KAHAWA MBINGA WATAKIWA KUJENGA MAZOEA YA KUTUMIA DAWA NA MBOLEA ZA ASILI


Hao ni wanakikundi cha Bagamoyo ambao hujishughulisha na kilimo cha zao la kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakifuatilia kwa umakini mafunzo juu ya matumizi ya viuatilifu asilia, kutoka kwa mtaalamu wa mimea na udongo Kaminyoge Mhamerd wa pili kutoka kushoto.





Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


MATUMIZI sahihi ya mbolea za asili katika uzalishaji wa zao la kahawa, imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha na kuongeza uzalishaji wa zao hilo, hivyo wakulima wametakiwa kujenga mazoea ya kutumia mbolea hizo mashambani mwao.

Pia uzalishaji wa zao hilo, inashauriwa kutumia dawa za asili ambazo humfanya mkulima kuvuna kahawa yenye kiwango cha juu na yenye ubora unaokubalika katika soko la dunia.

Rai hiyo imetolewa na mtaalamu wa mimea na udongo Kaminyoge Mhamerd wa kampuni ya Sustainable Harvest, ya kutoka wilaya ya Moshi mkoani kilimanjaro, ambayo hujishughulisha na uboreshaji wa zao hilo.



Kadhalika kampuni hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa mkulima wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, juu ya utengenezaji wa mbolea hizo za asili ambayo ina uwiano sahihi wa virutubisho vinavyotakiwa katika mmea wa kahawa na kutoa elimu namna ya kudhibiti ubora wa kahawa ikiwa shambani na kwenye mtambo wa kukobolea zao hilo.

Mhamerd alisema wamekuwa pia wakitoa utaalamu wa jinsi ya kudhibiti magonjwa na wadudu wanaoshambulia mmea wa kahawa ukiwa shambani, kwa kutumia viuatilifu asilia ambavyo havina madhara kwa mkulima mwenyewe na mazingira.

Alitolea mfano kwamba dawa moja wapo ya asili ambayo hutumika kuulia wadudu wanaoshambulia zao hilo kama vile vidung'ata na vidugamba, mkojo wa ng'mbe ambao huchanganywa na jivu na kuvundikwa ndani ya siku 14 ndio hutumika kupuliza kwa siku saba katika mashamba ya kahawa kwa ajili ya kuangamiza wadudu hao.

"Tangu tumeanza kuelimisha wakulima Mbinga, kumekuwa na mabadiliko kwa sababu wakulima wengi wamekuwa na uelewa wa kutosha juu ya matumizi sahihi ya njia za asili za kutunza zao la kahawa", alisema Mhamerd.

Pamoja na mambo mengine mtaalamu huyo wa mimea na udongo alieleza kuwa tokea waanze kutoa elimu hiyo bure, asilimia 58 ya wakulima wilayani Mbinga waliopata mafunzo hayo wamekwisha anza kutumia dawa hizo za viwatilifu na mbolea asilia.

Kutokana na hilo ubora wa uonjaji wa kikombe cha kahawa umeongezeka kutoka asilimia 83 hadi 86 katika vikundi vitano ambavyo vilifanya uzalishaji wa zao hilo kwa msimu wa kilimo wa mwaka jana ambapo vikundi hivyo ni Unango, Bagamoyo, Jitahidi, Lumeme na Jikwamue.

 

No comments: