Na Steven Augustino,
Songea.
ZAIDI ya watoto 53,000 wenye umri chini ya miaka mitano
mkoani Ruvuma, wanatarajiwa kupata chanjo mpya ya ugonjwa wa kichomi na
kuharisha mkoani humo.
Wakati taarifa za takwimu za magonjwa hayo zikitolewa,
zinaonesha kusababisha watoto takribani 6000 kupoteza maisha kila mwaka
na kushika nafasi ya pili na ya tatu kwa kusababisha vifo vingi vya watoto
yakitanguliwa na ugonjwa wa Malaria.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema hayo wakati
wa uzinduzi wa chanjo hizo za kuzuia ugonjwa wa kichomi na kuharisha, kwa
watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao umekuwa ukisababisha vifo
vingi kwa watoto hao.
Akizungumza katika uzinduzi wa chanjo hiyo mpya mkuu
huyo wa mkoa aliwaonya watu wanaowatisha akina mama ili wasiwapeleke watoto wao
kupata chanjo, kuacha vitisho hivyo mara moja na atakayebainika atachukuliwa
hatua za kiisheria.
Aidha katika tukio hilo Mwambungu, aliweza kuzindua
kwa kuwapa watoto matone ya dawa hizo za chanjo ambao walifikishwa katika
hospitali ya mkoa mjini Songea.
Na mkuu huyo wa mkoa alipomaliza zoezi hilo aliwahimiza
akina mama wenye watoto kuwapeleka katika vituo vya tiba ili wapate chanjo hiyo
mapema na wasikubali kurubuniwa au kudanganywa juu ya tiba za dawa hizo.
Awali mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Daniel
Malekela alimueleza mkuu huyo wa mkoa
kwamba maandalizi ya kutoa chanjo hiyo katika mkoa huo yamekamilika na kwamba
chanjo hiyo ni salama.
Dkt. Malekela alisema kuwa Chanzo hizo ni salama na
zimethibitiswa na Shirika la Afya Duniani(WHO) kuwa hazina madhara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya
kukamilika kwa uzinduzi wa chanjo hiyo, baadhi ya akina mama walisema wamepokea
kwa mikono miwili na kuwataka wenzao wajitokeze kwa kuwataka watoto wao
wapewe matone hayo ili wasishambuliwe na
magonjwa ya kichomi na kuharisha.
No comments:
Post a Comment