Wednesday, March 27, 2013

MWIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI ROSE MAHENGE KUTUMBUIZA WANAMBINGA SIKU YA SHEREHE ZA PASAKA


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


MWIMBAJI wa muziki wa Injili kutoka wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Rose Mahenge anatarajia kufanya uzinduzi wa albamu mpya iitwayo Waweza zeeka mapema, siku ya sikukuu ya Pasaka Machi 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa Uvikambi uliopo Mbinga mjini.

Akizungumza na Mtandao huu Mahenge anasema uzinduzi huo utashirikisha wasanii maarufu nchini, Senga na Pembe kutoka Jijini Dar es salaam ambao nao watakuwa wakitumbuiza na kutoa burudani za aina mbalimbali siku hiyo.

AKINA MAMA TUNDURU WALIA NA HUDUMA ZA AFYA


Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI imekumbushwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo, ili kuondoa kero ambazo zimekuwa zikilikabili kundi la wanawake na akina mama wajawazito, pale wanapohitaji kupatiwa huduma za matibabu na wakati wa kujifungua.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na baadhi ya wanawake walioshiriki katika vikundi vya kwaya, ngoma, maigizo na ngonjera zilizofanyika wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mchoteka wilayani Tunduru hapa mkoani Ruvuma.

MKUU WA WILAYA ALIA NA WANAOKWAMISHA MRADI WA USHOROBA, JESHI LA POLISI LAAGIZWA KUWACHUKULIA HATUA WAHUSIKA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JESHI la polisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, limeagizwa kuhakikisha kwamba linafanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu walioshiriki katika zoezi la hujuma za kubomoa jengo la mradi wa Ushoroba na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 36.9.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alitoa agizo hilo katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama, kilichoketi kwa ajili ya kujadili hasara za uharibifu wa mradi huo, ambao unajengwa kijiji cha Lukala kilichopo Kata ya Mchesi tarafa ya Lukumbule wilayani humo.

Alisema mradi huo unafadhiliwa na nchi ya Ujerumani, unajengwa ikiwa ni juhudi ya mwendelezo mradi wa ushirikiano wa kudhibiti vitendo vya ujangili, ambao umekuwa ukifanywa na wawindaji haramu katika nchi za Tanzania na Msumbiji.

WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO SHULE TUNDURU KUBURUTWA MAHAKAMANI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JUMLA ya kesi 1064 zinazowahusu wazazi na walezi walioshindwa kupeleka watoto wao shule, zimepangwa kuanza kusikilizwa ikiwa ni juhudi ya serikali kuhakikisha kuwa watoto wote waliochaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari, wanapelekwa shule.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, alisema hayo huku akifafanua kuwa, kesi zote zimepangwa kufanyika katika vijiji husika vya wilaya hiyo.

Nalicho alisema hali hiyo imetokana na wazazi hao kuendelea kukaidi maelekezo ya kupeleka watoto wao shule, hali               iliyoisukuma serikali kumtafuta hakimu, ambaye atahamishia shughuli za mahakama vijijini, ili kurahisisha kazi za utekelezaji wa sheria.

WANANCHI WA KATA YA NAMASAKATA TUNDURU WALILIA MAJI, WASEMA WAPO TAYARI KUTOA MTU KAFARA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATA ya Namasakata wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,  wametishia kutoa kafara ya mtu achinjwe, kwa ajili ya tambiko litakalosadia wananchi wa kata hiyo, kupata huduma ya maji safi na salama.

Diwani wa kata hiyo Masache Ally alisema hayo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Chande Nalicho, kufuatia adha kubwa wanayopata wananchi wake juu ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Alisema wamechoshwa na danadana na ahadi hewa zinazotolewa na serikali juu ya utekelezaji na utatuzi wa tatizo hilo.

Monday, March 25, 2013

MAKAA YA MAWE YAMPONZA GAUDENCE KAYOMBO, ATAMANI KUJIUZURU

Gaudence Kayombo Mbunge Mbinga Mashariki.


















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANANCHI siku zote wamekuwa wakiamini kwamba, kiongozi yeyote aliyewekwa madarakani, ni mtetezi na msimamizi mkuu wa maendeleo yao katika eneo husika.

Kana kwamba hilo halitoshi, baadhi yao wakishawekwa madarakani wanaonekana kuwa mwiba kwa wananchi, na hata kutotimiza ipasavyo majukumu yao ya kazi.

Jamii siku zote hufikia hatua ya kupoteza imani kwa viongozi wao endapo tu, pale wanapobaini msimamizi wao wa maendeleo tayari yupo katika mrengo wa kushoto dhidi yao, wakimuona akijijengea maslahi yake binafsi na kusahau wananchi anaowatumikia.

Tatizo hili likigundulika ndio maana utakuta migogoro au malalamiko ya hapa na pale huanza kujitokeza, na kiongozi husika kunyoshewa kidole wakati mwingine kusababisha kutokea kwa vurugu zinazoweza kuhatarisha amani katika eneo husika.

MALI ZA USHIRIKA MBICU UTATA MTUPU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga. 

KAMA serikali mkoani Ruvuma, haitachukua hatua za haraka katika kusimamia na kukabidhi kwa njia halali mali za chama cha ushirika MBICU kilichopo wilayani Mbinga mkoani hapa, hakika huenda wanachama wenye mali hizo wasinufaike nazo.

Kumekuwa na mgogoro mzito unaoendelea kufukuta hapa wilayani, kutokana na viongozi husika kudaiwa kukabidhi mali za ushirika huo kwa njia za siri, bila wanachama ambao ni wakulima wa ushirika huo kupewa taarifa kamili juu ya hatma ya mali zao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kwamba, MBICU ni chama cha ushirika kinachojumuisha wakulima wanaozalisha zao la kahawa wilayani Mbinga.

MIRADI YA UMWAGILIAJI MBINGA MASWALI MENGI KULIKO MAJIBU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

ENDAPO Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, itaendelea kupuuzia na kufumba macho juu ya usimamiaji na ujenzi bora wa miradi ya kilimo cha umwagiliaji, hakika maendeleo katika sekta ya kilimo hicho cha umwagiliaji hapa wilayani yataendelea kudorola.

Siku zote jamii imekuwa ikitambua kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote ile hapa duniani na ni tegemeo kwa wataalamu husika waliopo katika sekta hiyo, kuendeleza miradi mbalimbali ya kilimo hicho, ili wananchi wake hususani wakulima waweze kuzalisha mazao yao shambani kwa ubora unaokubalika.

Mwandishi wa makala haya anaelezea juu ya utata uliopo katika mradi wa umwagiliaji wa Sangamabuni uliopo kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi, ambapo umekuwa ukizua malalalamiko kutoka kwa wananchi kwamba ujenzi wake unashindwa kuendelea kutokana na uongozi wa wilaya hiyo, kushindwa kusimamia kikamilifu na kufuata taratibu husika za wataalamu wa kanda ya umwagiliaji Mtwara.

WALIA NA MWEKEZAJI WA MGODI WA MAKAA YA MAWE MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TANZANIA  ni nchi ambayo imejaliwa rasilimali nyingi ambazo zikitumika kwa ufasaha, taifa hili wananchi wake kwa asilimia kubwa wanaweza kuondokana na umasikini ambao umekuwa ukiitesa jamii nyingi miongoni mwao.

Lakini inashangaza kuona licha ya kuwa na rasilimali hizo kama vile madini ya aina mbalimbali, bado wananchi wake wamekuwa wakilalamika kila kukicha kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele.

Malalamiko hayo yamekuwa yakielekezwa hasa kwa viongozi wa serikali ambao ndio wamepewa dhamana na kusimamia misingi na taratibu nzuri ambazo zitamfanya Mtanzania aweze kunufaika nazo.

Chakusikitisha baadhi ya viongozi wetu ambao ndio wamepewa jukumu hilo, wanaonekana kutozingatia taratibu husika, na kusababisha kelele na hata maandamano yasiyokuwa ya lazima ambayo yanafanywa na wananchi wa eneo fulani ambako kero husika inatokea, yakilenga kudai haki zao.

Friday, March 1, 2013

WAZEE WA TUNDURU WAIJIA JUU CCM


Na Steven Augustino,
Tunduru.

BARAZA la wazee wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, limeazimia kufanya kikao cha dharula na kuiteua tume itakayo kwenda kuonana na Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya kikwete na kupeleka kilio na kero za wananchi wa wilaya hiyo.

Wakifafanua taarifa hiyo kwa nyakati tofauti Mwenyekiti mstaafu wa CCM wilaya hiyo Kanduru Kassim,  na mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kapopo walisema kuwa hali
hiyo imetokana na kuwepo kwa tabia za viongozi wa chama na serikali wilayani humo, kupuuza kero na malalamiko ya wananchi wa wilaya hiyo.

Walisema licha ya malalamiko hayo ambayo yanafahamika, lakini chama na serikali vikiwa vimekaa kimya, hivyo baraza hilo limeadhimia kukutana na kuainisha kero zote na kuzianisha tayari kwa safari hiyo zikiwa ni juhudi za kukinusuru chama cha mapinduzi.

BWANA AFYA TUNDURU KUKIONA CHA MOTO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

CHAMA cha Wanachi CUF kimetoa siku 14 kumtaka Bwana afya wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kutoa kibali cha kufungua Mbesa Hoteli iliyopo mjini humo, vinginevyo watafanya maandamano hadi katika ofisi za Mkuu wa wilaya hiyo kushinikiza hoteli hiyo ifunguliwe.

Tamko la kutaka kufanya maandamano hayo, lilitolewa katika mkutano wa kumkumbuka mwanzilishi na Mwalimu wa Siasa wilayani humo, marehemu Mazee Rajab aliyefariki Februari 17 mwaka 2010, uliofanyika katika viwanja vya Baraza la Idd mjini Tunduru.


Lengo la kumtaka mkuu huyo wa wilaya Chande Nalicho kufungua hoteli hiyo inatokana na kile kinachodaiwa kuwa, hoteli hiyo iliyopo katika mji huo imefungwa kwa njia ya uonevu.