Na
Kassian Nyandindi,
Songea.
UJENZI wa barabara kiwango
cha lami kuanzia eneo la Likuyufusi pacha ya Peramiho wilaya ya Songea hadi
Mbinga, umeanza kuzua malalamiko kutokana na barabara hiyo kuanza kuwekwa
viraka kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.
Barabara
hiyo ambayo ni ya kilometa 78 inagharimu kiasi cha shilingi bilioni 79.8 na kutekelezwa
chini ya mradi mkuu wa changamoto za milenia Tanzania (MCAT).
Fedha
za ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni mwa dola 698 za Kimarekani zilizotolewa
nyakati za mwisho katika utawala wa Rais mstaafu George Bush, ikiwa ni sehemu
ya msaada kwa ajili ya kujenga miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini.
Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati
tofauti wakati mwandishi wa habari hizi alipokuwa akizungumza na wananchi wa
Songea na Mbinga, ambapo walisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona ujenzi wa
barabara hiyo kabla haijakabidhiwa rasmi imeanza kuwekwa viraka baadhi ya
maeneo.