Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu
amekipongeza chuo kikuu cha sayansi ya kompyuta cha Mtakatifu Joseph tawi la
Songea mkoani humo, kwa jitihada zake za kuendelea kupanua wigo wa kutoa huduma
na kukuza elimu ya juu hapa nchini.
Mwambungu alitoa pongezi hizo alipokuwa
akihutubia kwenye mahafali ya tano ya chuo hicho mjini hapa, kwa wahitimu 119
wa shahada na stashahada ambapo alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho,
kumesaidia kulipunguzia taifa tatizo la ukosefu wa wataalam wa sayansi hususan
katika ukanda wa kusini na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo kikuu cha
sayansi ya kilimo na teknolojia katika sekta ya kilimo, ni jambo jema kwa
ustawi wa nchi na uti wa mgongo na mwajiri mkubwa kwa wananchi huku akiwataka
wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika
jamii.
Alieleza kuwa katika maisha ya sasa hakuna njia
fupi ya kufikia mafanikio katika maisha zaidi ya kufanya kazi kwa bidii
na maarifa, na kwamba changamoto zilizopo katika chuo hicho zigeuzwe kuwa fursa
pekee ya kujipanua na kutoa elimu bora, huku akiwataka kuboresha
mawasiliano ili kukuza wigo wa utatuzi wa changamoto hizo.