Tuesday, May 7, 2013

MKUU WA MKOA WA RUVUMA NA WAKURUGENZI WA TAKUKURU WAKIFUATILIA SEMINA YA RUSHWA ILIYOHUSISHA VIONGOZI WA DINI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu upande wa kushoto na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Edward Hosea na upande wa kulia ni  Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma, Daudi Masiko wakifuatilia semina ya Rushwa iliyohusisha viongozi wa Dini kutoka Nyanda za juu kusini, inayofanyika leo kwenye ukumbi wa Heritage uliopo mjini Songea.(Picha na Mwandishi wetu)

MKURUGENZI WA TAKUKURU AWASILI RUVUMA, AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUELIMISHA WAUMINI WAWE WAADILIFU NA KUACHANA NA VITENDO VYA RUSHWA

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) Dokta Edward Hosea amewasili hapa mkoani Ruvuma, na kuwataka viongozi wa dini kuendeleza dhana ya kutambua kuwa Rushwa ni miongoni mwa dhambi inayokatazwa katika vitabu vya dini, na badala yake kuwakumbusha waumini wao kutenda mema na kuwa waadilifu.(Picha na Mwandishi wetu)

WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AKIWAPA POLE BAADHI YA MAJERUHI KATIKA HOSPITALI YA MOUNT MERU JIJINI ARUSHA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwapa pole baadhi ya majeruhi wa bomu la kutupwa kwa mkono lililolipuka katika kanisa Katoliki la Olasiti Jijini Arusha, wakati alipowatembelea kwenye hospitali ya mkoa wa Arusha leo, Mount Meru(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 













WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA ATEMBELEA LEO KANISA KATOLIKI LA OLASITI, LENGO KUZUNGUMZA NA WAUMINI NA VIONGOZI WA KANISA HILO, KUWAPA POLE

Waziri mkuu Mizengo Pinda akizungumza na Waumini wa kanisa katoliki la Olasiti Jijini Arusha leo, alikokwenda kutoa pole kufuatia mlipuko wa bomu la kutupwa kwa mkono, uliotokea kanisani hapo May 6 mwaka huu, na kusababisha vifo na majeruhi.(Picha na Mwandishi wetu).


Na Mwandishi wetu,
Arusha.

PAMOJA mambo mengine Waziri mkuu Pinda, aliwataka waumini wa kanisa hilo, katika kipindi hiki kigumu kuwa watulivu na kuendelea kumuomba Mungu, wakati serikali inaendelea na mchakato wa kulishughulikia tatizo hili.

Kadhalika Waziri huyo alilaani kitendo hicho cha kinyama kilichofanywa, na kuongeza kuwa serikali haitokubali kuendelea kuvumilia matukio kama haya kuendelea kutokea hapa nchini.

Mungu ibariki Tanzania, tuepushe na majanga kama haya wenye nia mbaya na nchi yetu, walaaniwe.

WASAUDI ARABIA MBARONI, WADAIWA KUHUSIKA NA TUKIO LA BOMU ARUSHA

                      Daktari wa Hospitali ya Mount Meru Jijini Arusha,      akimuhudumia mtoto aliyepigwa na bomu. 
Na Mwandishi wetu,

WAKATI Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, akikatisha ziara yake nchini Kuwait, kurudi hapa nchini kwa lengo la kuungana na Watanzania wenzake katika kipindi hiki kigumu, Jeshi la Polisi  linawashikilia watuhumiwa kadhaa kwa madai ya kuhusika na mlipuko wa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu, lililorushwa siku ya Jumapili katika Kanisa katoliki la Olasiti Jijini Arusha.
Miongoni mwa washukiwa ambao wako mikononi mwa polisi ni raia wanne wa Saudi Arabia na wengine wanne ni raia wa Tanzania. 

Monday, May 6, 2013

SHAMBULIO LA KIGAIDI LILILOTOKEA ARUSHA, RAIS AKATIZA ZIARA YAKE NCHINI KUWAIT

 


 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Mei 6, 2013, ameamua kukatiza ziara yake ya Kiserikali nchini Kuwait ili kurejea nyumbani kutokana na tukio la shambulio la kigaidi la mlipuko mjini Arusha ambako watu wawili wamefariki na 60 wamejeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ya Dar es Salaam, imesema Rais Kikwete aliyekuwa aondoke arejee nyumbani kesho, amelazimika kukatiza ziara hiyo na anaondoka Kuwait City kurejea nyumbani mara moja ili kuwa karibu na wafiwa pamoja na wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.

Miongoni mwa shughuli ambazo hazitafanyika sasa kutokana na uamuzi huo wa Rais ni ziara ya kutembelea Kampuni ya Mafuta ya Kuwait katika  eneo la Ahmadi mjini Kuwait. Aidha, Rais hatahudhuria dhifa ya chakula cha jioni ambacho alikuwa anaandaliwa na Waziri Mkuu wa Kuwait, Mheshimiwa Sheikh Jaber Al Mubarak Al Hamad Al Sabah.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Mei, 2013

 

MWEKEZAJI MGODI WA MAKAA YA MAWE MBINGA ARUHUSIWA KUENDELEA NA KAZI, MKUU WA MKOA AKIRI WANANCHI KUNYWA MAJI YENYE SUMU

Mtambo maalum, ukifanya kazi ya kuchimba makaa ya mawe huko kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi

Mbinga.

MGODI wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma ambao ulifungwa kwa muda usiojulikana sasa umefunguliwa rasmi, na mwekezaji husika ameruhusiwa kuendelea na shughuli za uchimbaji wa makaa hayo.

Ufunguzi huo umefanyika hivi karibuni Mei 3 mwaka huu majira ya mchana na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, ambaye ndiye aliyeufunga Aprili 30 mwaka huu.

Mwambungu alitoa kauli ya kuufungua mgodi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa eneo la ofisi za kijiji cha Ntunduaro, ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya ya Mbinga  na mkoa wa Ruvuma, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.

KANISA KATOLIKI OLASITI KULIPOTOKEA MLIPUKO HUKO ARUSHA NI HILI HAPA


JUU YA TUKIO LA ARUSHA, RAIS KIKWETE LAMSIKITISHA



                        

                 THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha.  Tukio hilo la kigaidi limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa.  

Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu wake. 
Rais Kikwete ameagiza vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.  Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.  Tutawasaka popote walipo na kupambana nao bila huruma.  

Aidha, tutakabiliana na aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu.  Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
 5 Mei, 2013

Friday, May 3, 2013

MKUU WA MKOA WA ARUSHA ATISHIA WAANDISHI WA HABARI, ASEMA ATAKAYEIGUSA SERIKALI ATAKUWA AMEIWEKA ROHO YAKE REHANI

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo.


















Na Mwandishi wetu,

Arusha.

MKUU wa mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo ametoa onyo kali kwa waandishi wa habari nchini, kwamba yeyote atakayeishambulia na kuikosoa au kuigusa serikali atakiona cha mtema kuni.

Mulongo amesema yupo tayari kushirikiana na waandishi wa habari Tanzania, lakini atakaye thubutu kuigusa serikali atakuwa ameiweka roho yake rehani.

Mpaka sasa haijafahamika kwa nini RC huyo ametoa kauli hiyo, lakini wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kwamba Mulungo amelazimika kutoa kauli hiyo kutokana na kutofautiana na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ambaye sasa ameshitakiwa kwa uchochezi.

Thursday, May 2, 2013

MGODI WA MAKAA YA MAWE NGAKA, WAFUNGWA WANANCHI WAMTAKA MBUNGE WA MBINGA MASHARIKI AJIUZURU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Matrekta yakifanya kazi ya kuchimba mkaa wa mawe katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu,  amelazimika kuufunga kwa muda usiojulikana, mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoani humo, baada ya wananchi wa kijiji hicho kumtaka mkuu huyo wa mkoa aufunge mgodi huo mpaka watakapolipwa madai yao ya muda mrefu ya fidia wanazodai, pamoja na kuyaweka mazingira yao katika hali inayostahili kwa matumizi ya binadamu.

Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC, na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

Mwambungu alichukua uamuzi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Ntunduaro, ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya ya Mbinga  na Mkoa wa Ruvuma, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.

TUNDURU SEKTA YA ELIMU BADO KUNA MATATIZO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MADIWANI wameiomba Serikali kuwabana baadhi ya walimu wa shule za Msingi na Sekondari, wanaoendesha miradi ya kuonesha picha za video katika maeneo ya shule, huku wakieleza kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya maendeleo ya elimu kwa watoto wao.

Hayo yalisemwa na diwani wa viti maalum katika kata ya Nalasi Alus Yunusi, ambaye alisema kutokana na hali hiyo walimu hao wamekuwa hawazingatii maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi, zaidi ya kuangalia maslahi yao yatokanayo na miradi hiyo.

Akifafaa taarifa hiyo Yunusi alisema kuwa hayo ameyabaini katika tarafa yake, ambapo biashara hiyo ya kuonyesha picha za video imekithiri na kwamba endapo watafumbiwa macho taaluma katika wilaya hiyo itaendelea kuporomoka.

Tuesday, April 30, 2013

MWANTUMU BAKARI MAHIZA ATEULIWA KUWA SKAUTI MKUU TANZANIA

Mheshimiwa Mwantumu Mahiza.

























Na Mashirika Mbalimbali ya habari,
Dar es Salaam.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Mwantumu Bakari Mahiza kuwa Skauti mkuu nchini.

Kwa mujibu wa barua ya Katibu mkuu kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa, uteuzi wa Mahiza umeanza tangu Aprili 19 mwaka huu.

Mahiza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kanali mstaafu Iddi Kipingu, ambaye amemaliza muda wake.

                                     Imetolewa na:

          Kaimu Katibu mkuu, Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi.

GODBLESS LEMA ALIA NA POLISI, ASIMULIA JINSI WALIVYOMVAMIA NYUMBANI KWAKE

Umati wa watu ukiwa umejaa nje ya jengo la Mahakama Arusha, kusikiliza kesi ya Lema.



















Na Waandishi wetu,
Arusha.

MBUNGE wa Arusha mjini Godbless Lema kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) ambaye amechiwa huru kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa huo, amewataka wanachama wa chama hicho kumzomea mkuu wa mkoa wa Arusha Magessa Mulongo kila watakapomuona.

Pia Lema amesimulia jinsi alivyovamiwa nyumbani kwake, usiku wa kuamkia Aprili 26, mwaka huu.

Lema akiwa amefuatana na wafuasi na wanachama wa Chadema walikusanyika katika viwanja vya Ngarenaro ambako mbunge huyo aliwahutubia kwa dakika kadhaa na kuwataka wafuasi wake warejee nyumbani.

WANAFUNZI WAFARIKI DUNIA KWENYE DIMBWI LA MAJI

Na Mwandishi wetu,
Tarime.

WANAFUNZI wawili wanaosoma darasa la sita wilayani Tarime, wamekutwa na mauti baada ya kuzama katika dimbwi lenye tope na maji mengi.

Wanafunzi hao ni wa shule ya msingi Nyamwaga, katika kijiji cha Nyakunguru, kata ya Kibasuka wilayani humo.

MWALIMU MSTAAFU AFARIKI DUNIA KWA KUNYWA GONGO

Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki




















Na Steven Augustino,
Tunduru.

MWALIMU mstaafu katika kijiji cha Kidodoma wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma Rajab Mohamed Kalesi (65) amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kunywa pombe haramu ya gongo.

Mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mdogo wa marehemu  Athuman Saidi walisema kuwa kabla ya mkasa huo, marehemu huyo alionekana akinywa Pombe hiyo kwa siku mbili mfululizo, huku akiwa amejificha katika nyumba ya muuzaji wa pombe hiyo Hamdi Swalehe.

Habari zinaeleza kuwa mwalimu huyo kabla ya kukutwa na mauti, alikuwa akiwa anatamba kuwa na fedha nyingi, alizokuwa ametoka kulipwa kama mafao ya kustaafu kazi hiyo.

Monday, April 29, 2013

WARIOBA: ITATOLEWA KATIBA YENYE MASLAHI YA TAIFA

Kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Assaa Rashid. (Picha na Tume ya Katiba)


















Dar es Salaam, 
Tanzania.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba LEO imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013).

Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema lLEO (Jumatatu, Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.

“Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa  na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni.

Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.

 Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu:

Akizungumza kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.

Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.

Jaji Warioba amesema Baraza moja litaundwa Tanzania Bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.

“Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote,” amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo zinaonyesha baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji, vitongoji na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.

 Chaguzi za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya:

Aidha, Jaji Warioba amezungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi karibuni za kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini ya Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.

“Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huu, hali kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339 kwa Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa Mwongozo,” amesema Jaji Warioba.

Kuhusu hatua inayofuata baada ya chaguzi hizo, Jaji Warioba alisema Tume inaendela kupokea majina kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na ya wananchi wote waliopendekezwa kutoka katika Kata na Shehia na kazi hiyo inatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013).

Changamoto:

Akizungumzia kuhusu changamoto zilizojitokeza katika chaguzi hizo, Jaji Warioba amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa na misimamo ya kisiasa na kidini

“Katika baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufangamanisha chaguzi za Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya kisiasa na kidini,” amesema Jaji Warioba.

Jaji Warioba ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya rushwa katika chaguzi hizo ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo ya katiba.

 “Tumepokea pia malalamiko ya vitendo vya rushwa,” alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo zinapaswa kushughulikia malalamiko hayo.

 Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba:

Katika mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa na Tume.

Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza haya yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.

“Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” alisema Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa.

BREAKING NEWS: MWANAFUNZI AKATWA MKONO, AUGUZA JERAHA HOSPITALINI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MWANAFUNZI anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Mwongozo kata ya Ligoma tarafa ya Namasakata wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,  ameumizwa vibaya katika mkono wake wa kulia baada ya kukatwa na upanga na mwanafunzi mwenzake.
Ikra Said mwenye umri wa miaka saba ndiye aliyekatwa mkono wake, na amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Tunduru akiendelea na matibabu.

Mwandishi wa habari hizi amezungumza na majeruhi huyo ambapo alisema  kuwa mkasa huo ulimpata wakati akiwa na wanafunzi wenzake ambao walikuwa wametumwa na mwalimu waliye mtaja kwa jina moja la Komba ili wakamtafutie kuni msitu uliojirani na shule hiyo.

Akifafanua taarifa hiyo mwanafunzi huyo alisema kuwa wakati wakiwa katika harakati hizo za kutafuta kuni, ghafla alijikuta akishambuliwa kwa kukatwa na panga katika mkono wake wa kulia, na mwanafunzi mwenzake Ashraki Said anayesoma darasa la tatu shuleni hapo.   

Friday, April 26, 2013

MWAMBUNGU: WATENDAJI AMBAO NI KIKWAZO CHA MAENDELEO RUVUMA NITAWAFUKUZA KAZI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.



















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WATENDAJI wa serikali katika Halmashauri za mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kufanya kazi zao ipasavyo kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, na kwa yule atakayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufukuzwa kazi.

Vilevile mtendaji atakayeonekana kuwa kikwazo katika shughuli za kimaendeleo ya wananchi, hatavumiliwa badala yake atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa fikishwa mahakamani.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, alipokuwa akihutubia katika Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo lililoketi leo kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Friday, April 19, 2013

MAKAMPUNI YANAYOKIUKA TARATIBU ZA UNUNUAJI WA KAHAWA MBINGA YAANDALIWA MWAROBAINI

Gaudence Kayombo, Mbunge wa Mbinga Mashariki.



















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BODI ya kahawa kanda ya Ruvuma, imeagizwa kufanya ufuatiliaji wa karibu juu ya makampuni yanayojiandikisha majina mawili tofauti na kujihusisha na ununuzi wa zao hilo, kwa wakulima vijijini na mnadani Moshi ili yachukuliwe hatua za kisheria.

Agizo hilo lilitolewa katika kikao cha wadau wa kahawa mkoani humo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki uliopo Mbinga mjini, ambapo ilielezwa kuwa makampuni yanayofanya hivyo yanamuumiza mkulima na wafanyabiashara wadogo wadogo.

Kufuatia agizo hilo kampuni ya Tutunze ambayo inajishughulisha na ununuaji wa kahawa wilayani Mbinga, ilinyoshewa kidole na wadau hao kwamba inaongoza kwa ukiukaji wa taratibu za ukoboaji wa kahawa mbivu mitamboni huko vijijini.