Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
MWALIMU mstaafu katika kijiji
cha Kidodoma wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma Rajab Mohamed Kalesi (65) amekutwa
akiwa amefariki dunia baada ya kunywa pombe haramu ya gongo.
Mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mdogo wa
marehemu Athuman Saidi walisema kuwa kabla ya mkasa huo, marehemu huyo alionekana
akinywa Pombe hiyo kwa siku mbili mfululizo, huku akiwa amejificha katika
nyumba ya muuzaji wa pombe hiyo Hamdi Swalehe.
Habari zinaeleza kuwa
mwalimu huyo kabla ya kukutwa na mauti, alikuwa akiwa anatamba kuwa na fedha
nyingi, alizokuwa ametoka kulipwa kama mafao
ya kustaafu kazi hiyo.
Walisema kufutia taarifa
hiyo ya kupokea fedha hizo anadaiwa kuwa na fedha zaidi ya shilingi milioni
48, alionekana kutembea na wapambe muda wote huku wakienda kujipatia kinywaji
hicho kwa wingi, na kumsababishia kupoteza uhai wake.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti Diwani wa viti maalumu wa tarafa ya Nampungu Rehema Nyoni na mtendaji
wa kijiji hicho, Mbuyu Allky Mbuyu walisema kuwa baada ya wapambe wake kuona
hali ya mwalimu huyo inabadilika walitokomea kusikojulikana, na kumuacha peke
yake katika nyumba ya muuza pombe hiyo hadi mauti yalipomkuta.
Walisema akiwa katika hali
ya kutapatapa mke wa muuza pombe alijitahidi kuokoa maisha yake kwa kumpatia
huduma ya kwanza kwa kumpepea, na kumwagia maji ya baridi huku akimnywesha uji,
lakini hali ilizidi kuwa mbaya na alipokata roho mumewe
Hassani Swalehe
alitimua mbio na kumwacha marehemu akiwa peke yake.
Akizungumzia tukio hilo mganga aliyeufanyia
uchunguzi mwili wa marehemu huyo Dokta Goerge Chiwangu alisema, chanzo cha kifo
hicho kilisababishwa na unywaji wa pombe nyingi.
Kamanda wa polisi mkoa wa
Ruvuma Deusdedith Nsimeki amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo,
na kuongeza kuwa jeshi la polisi linamshikilia mke wa muuza pombe hiyo haramu, ambaye
hakumtaja jina lake
kwa ajili ya uchunguzi.
No comments:
Post a Comment