Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kujenga
ushirikiano na sio kujengeana ubaguzi, ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kusukuma mbele gurudumu la kimaendeleo
kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Sambamba na hilo wametakiwa kushiriki kikamilifu katika suala
zima la ulinzi na usalama, ili wilaya hiyo iweze kuwa na amani na utulivu na
hatimaye wananchi wilayani humo, waweze kuishi kwa raha mustarehe bila kuwepo
vikwazo vya hapa na pale.
Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi
wa albamu ya nyimbo za injili, ‘Waweza
zeeka mapema’ iliyotungwa na mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili wilayani humo Rose Mahenge, uzinduzi ambao
ulifanyika kwenye ukumbi wa Uvikambi uliopo Mbinga mjini.
Senyi Ngaga alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa albamu hiyo ambayo
imesheheni nyimbo hizo, zenye kufunza wanadamu waishi kwa upendo na amani,
sio kupenda mambo ambayo hayampendezi mwenyezi Mungu.
Kadhalika uzinduzi huo ulishirikisha wasanii maarufu nchini,
Senga na Pembe wa kutoka Jijini Dar es salaam, ambao nao walikuwa wakitumbuiza
na kutoa burudani za aina mbalimbali.
Albamu hiyo imebeba nyimbo lukuki za kumsifu Mungu ambazo ni Waweza zeeka mapema,
Mbinguni tutaimba, Maajabu ya wanadamu, Leleno tuhine, Nasubiri zamu yangu,
Mungu nikupe nini, Uumbaji wa Mungu, Makabila yote, Rimix(Mbinguni tutaimba) na
Mwanaume ni Yesu.
Hiki ni kibao cha pili kutolewa na msanii huyo maarufu wa
nyimbo za injili hapa wilayani Mbinga, ambapo awali aliweza kutoa kibao kingine
ambacho kilitamba kwa jina la ‘Mbinguni
ndiko nyumbani kwetu’.
Kwa mujibu wa maelezo ya msanii huyo alimweleza mwandishi wa
habari hizi kuwa, nyimbo hizo zimebeba maudhui yanayolenga na kumtaka binadamu
kumcha Mungu na kuacha starehe na anasa mbalimbali ambazo zimekuwa
zikisababisha ongezeko la dhambi duniani.
Awali Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, aliwasisitiza
wakazi wa wilaya hiyo kuzingatia suala la elimu, ikiwemo kwanza kupeleka watoto
wao shule, ndipo mambo mengine ya kimaendeleo yafuate na kuacha tabia ya kuendekeza
kuchangia kwenye harusi au sherehe za aina mbalimbali.
No comments:
Post a Comment