Na
Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI
mmoja wa kijiji cha Daraja mbili kata ya Namwinyu tarafa ya Matemanga wilayani
Tunduru mkoani Ruvuma, Chalamanda Masapi
(65) amefariki dunia baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na Tembo.
Taarifa
za tukio hilo zinaeleza kuwa marehemu Masapi alikumbwa na mkasa huo
baada ya kukutana na tembo huyo ambaye alikuwa na mtoto, ghafla wakati
akikagua uharibifu wa mazao uliofanywa na kundi la wanyama hao, katika shamba
lake lililopo nje kidogo na kijiji hicho.
Mtoto
wa marehemu Chalamanda ambaye alikuwa ni miongoni mwa shuhuda wa tukio hilo
Rashid Chalamanda alisema, yeye na marehemu baba yake kwakushirikiana na
kundi la wananchi wanaolima katika eneo hilo, walikwenda katika mashamba yao
kushiriki katika zoezi la kuwafukuza tembo hao ambao pia walivamia kijijini
hapo na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao yao.
Alisema
katika tukio hilo la kushitukiza marehemu alijikuta akiwa mikononi mwa
mnyama huyo, ambaye baada ya kumkamata
kwa kutumia mkonga wake alimrusha juu na kukinga katika mti uliokuwa
karibu na eneo hilo, kabla ya kumkanyaga na kumsaga na baadae kumpiga kwa
kutumia pembe zake na kumtoboa toboa vibaya mbavuni na tumboni.
Akizungumzia
tukio hilo afisa wanyama pori
wa wilaya hiyo Peter Mtani pamoja na kukiri kuwepo kwa tukio hilo, alisema kuwa tayari idara yake
imepeleka askari wenye silaha ili waende kuandaa mtego, ambao utafanikisha
kuuawa kwa tembo huyo.
Mtani
aliendelea kueleza kuwa matukio ya tembo hao kuvamia na kufanya uharibifu
katika mashamba ya wakulima wa Tunduru, yamekuwaa yakijitokeza mara kwa mara na
kwamba kutokana na hali hiyo idara yake imekuwa ikifanya kazi ya ziada
kuwafukuza wanyama hao, ili wasiendelee kuharibu mazao ya watu.
Alisema
pindi inapobainika kuwa tembo hao wanazidi kufanya mashambulizi ya kuua watu idara
hiyo pia imekuwa ikichukua hatua za kuwasaka na kuwaua tembo hao haraka
iwezekanavyo ili wasiweze kusababisha madhara kwa watu wengine.
Akizungumzia
hali na muonekano wa mwili wa marehemu huyo mmoja kati ya waganga wa hospitali
ya wilaya ya Tunduru, Dkt. George Chiwangu alisema kuwa marehemu
alifariki dunia kutokana na kutokwa na damu nyingi zilizosababishwa na kutobolewa
matundu manne ubavuni na tumboni.
Dkt.George
Chiwangu aliendelea kueleza kuwa sambamba na hali hiyo pia mwili wa
marehemu ulikutwa ukiwa umevurugika vibaya huku shingo yake ikiwa imevunjika na
kichwa kupasuka.
No comments:
Post a Comment