Na Steven Augustino,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,
imeahidi kutoa msaada wa shilingi milioni 2.8 katika kituo cha kulelea watoto
yatima, kinachomilikiwa na Kanisa la Bibilia kijiji cha Mbesa wilayani
humo ikiwa ni juhudi yake ya kujali watoto hao.
Ahadi hiyo ilitolewa na Mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri hiyo Robert Nehatta wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya
Wanawake wa kikristo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Tayari fedha hizo zimekwisha pewa Baraka na Baraza la
madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo na kupitishwa katika bajeti ya mwaka
2013/2014.
Nehatta ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho
hayo alilazimika kutoa kauli hiyo kufuatia maombi yaliyotolewa na Umoja wa
wanawake wa Kikristo wilayani Tunduru, ambao pamoja na mambo mengine
walibainisha kuwa hivi sasa kituo hicho kinalea watoto wachanga ambao hufiwa na
mama zao wakati wa kujifungua, kwamba kipo katika hali mbaya kiasi cha kutishia
kufungwa baada ya wafadhili kutoka Ujerumani kusitisha kutoa misaada.
Kufuatia kauli hiyo pia waumini waliohudhulia katika
ibada hiyo wakajikamua kwa hali na mali kupitia mfumo wa changizo la papo kwa
papo na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 210,000 ili kuwasaidia watoto
hao.
Awali akisoma taarifa ya hali mbaya inayoikabili kituo
hicho katibu wa kikundi hicho Sara Samatta alimweleza mgeni huyo kuwa hayo yalibainika
wakati umoja huo, ulipokitembelea kituo hicho mwanzoni mwa mwaka huu ambapo
pamoja na mambo mengine walibaini kupungua kwa kasi ya kupokea watoto hao kutokana
na hali mbaya inayowakabili, ambapo kwa sasa kinapokea idadi ya watoto 30 tu
kati ya 60 waliokuwa wakipokelewa awali tangu kituo hicho kianzishwe mwaka
1960.
Alisema katika ziara hiyo ambayo wanakikundi hao
walitoa msaada wa vitu mbalimbali vyenyethamani ya shilingi 230,000
zilizotokana na michango ya waumini wa makanisa ya kikristo wilayani Tunduru, pia
walibaini kuwepo kwa mahitaji makubwa ya msaada katika kituo hicho cha kulelea
watoto yatima.
Kupitia maombi hayo pia umoja wa wanawake hao ulitumia
nafasi hiyo kuwaomba watu wenye uwezo, mashirika na makundi mbalimbali
kukiangalia kituo hicho kwa jicho la huruma kwa kutoa misaada ya hali na mali,
ili kuwaokoa watoto hao wenye mahitaji makubwa ya mapenzi ya wazazi
katika katika kulelewa kwao.
No comments:
Post a Comment