Friday, April 19, 2013

MAKAMPUNI YANAYOKIUKA TARATIBU ZA UNUNUAJI WA KAHAWA MBINGA YAANDALIWA MWAROBAINI

Gaudence Kayombo, Mbunge wa Mbinga Mashariki.



















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BODI ya kahawa kanda ya Ruvuma, imeagizwa kufanya ufuatiliaji wa karibu juu ya makampuni yanayojiandikisha majina mawili tofauti na kujihusisha na ununuzi wa zao hilo, kwa wakulima vijijini na mnadani Moshi ili yachukuliwe hatua za kisheria.

Agizo hilo lilitolewa katika kikao cha wadau wa kahawa mkoani humo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki uliopo Mbinga mjini, ambapo ilielezwa kuwa makampuni yanayofanya hivyo yanamuumiza mkulima na wafanyabiashara wadogo wadogo.

Kufuatia agizo hilo kampuni ya Tutunze ambayo inajishughulisha na ununuaji wa kahawa wilayani Mbinga, ilinyoshewa kidole na wadau hao kwamba inaongoza kwa ukiukaji wa taratibu za ukoboaji wa kahawa mbivu mitamboni huko vijijini.

Walisema kampuni hiyo imekuwa na tabia ya kukusanya kahawa majira ya jioni na kuilaza nyakati za usiku bila kukobolewa, hivyo kusababisha kupungua ubora wake.

“Kampuni hii inamilikiwa na wazungu, wamekuwa wakinunua kahawa hapa Mbinga kwa njia za ujanja, hawatusaidii wakulima badala yake wanatuangamiza, tunaiomba serikali ichukue hatua dhidi ya kampuni hii”, alisema Fidelis Mwaipopo.

Naye Blanka Ndunguru alisisitiza kwamba makampuni mengi ya kigeni yanayokuja kununua zao hilo mkoani Ruvuma, yamekuwa hayafuati kanuni kumi za uandaaji wa kahawa, hivyo mkulima kumsababishia hasara na hawaoni sababu ya makampuni hayo kuendelea kufanya biashara hiyo.

Sambamba na hilo wadau hao walijiwekea mikakati kwamba, taasisi zinazojishughulisha na uendelezaji wa zao hilo zifanye shughuli ya kuendelea kuelimisha wakulima wanaolima kahawa katika wilaya zote za mkoa humo, ili waweze kuzalisha kwa ubora unaokubalika na masoko ya kimataifa.

Vilevile ilishauriwa kuhimiza wakulima kutumia soko la ndani badala ya kutegemea masoko ya nje, ili kuwa na uhakika wa kuuza kahawa yao na kupata malipo yao kwa wakati.

Awali Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alisema, serikali wilayani humo itafuatilia kwa umakini  tatizo la makampuni yanayonunua kahawa kutofuata taratibu zilizowekwa, na ile itakayobainika itachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa makampuni mengine yenye tabia ya kuvunja taratibu husika.


No comments: