Friday, April 26, 2013

MWAMBUNGU: WATENDAJI AMBAO NI KIKWAZO CHA MAENDELEO RUVUMA NITAWAFUKUZA KAZI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.



















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WATENDAJI wa serikali katika Halmashauri za mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kufanya kazi zao ipasavyo kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, na kwa yule atakayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufukuzwa kazi.

Vilevile mtendaji atakayeonekana kuwa kikwazo katika shughuli za kimaendeleo ya wananchi, hatavumiliwa badala yake atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa fikishwa mahakamani.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, alipokuwa akihutubia katika Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo lililoketi leo kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.


Sambamba na hayo Mwambungu, aliwaagiza pia wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini, inajengwa kwa viwango bora na sio vinginevyo.

“Mradi laz\ima ujengwe kwa ubora unaofaa, ujenzi wa miradi mibovu unasababisha hasara kwa wananchi, ni lazima fedha za serikali zisitumike kama kichwa cha mwendawazimu zifanye kazi kwa umakini”, alisema.

Aidha aliinyoshea kidole wilaya ya Mbinga, kwa kile alichoeleza kuwa kuna matatizo katika maendeleo ya sekta ya elimu, hivyo viongozi husika wanatakiwa kukaa chini na kulifanyia upembuzi yakinifu.

“Mbinga kuna matatizo makubwa kwenye elimu hali yenu ni mbaya mno, kama kila mmoja wetu atadhamiria tubadilike kwenye elimu tutafikia malengo na lazima tujiulize kwa nini tupo nyuma?”, alisema Mwambungu.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa matatizo hayo katika sekta hiyo muhimu yanasababishwa na baadhi ya watu kuwapa mimba watoto wa kike na kusababisha mtoto husika kutoendelea na masomo.

“Natoa agizo juu ya jambo hili, kuna tetesi baadhi ya wafanyakazi wa serikali nao wanashiriki kuwajaza mimba wanafunzi wa kike, naagiza kwa yule ambaye anahisiwa kufanya vitendo hivi nipeni taarifa atakamtwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo hata kufukuzwa kazi”, alisisitiza.

Hata hivyo aliwaasa viongozi wa mkoa wa Ruvuma, wasiwe wachochezi katika kushawishi vurugu au machafuko katika jamii badala yake wafanye watu waishi kwa amani.




No comments: