Ziwa Nyasa. |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
YAMEJITOKEZA
maafa makubwa wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha wilayani humo, na
kusababisha mtu mmoja kufariki dunia, mazao yaliyolimwa shambani na mifugo
kusombwa na maji.
Tukio
hilo limetokea
usiku wa tarehe 14 mwaka huu, ambapo watu wamekosa mahali pa kuishi kutokana na
nyumba zao kujaa maji na kulazimika, kwenda kuomba msaada kwa majirani wenzao.
Akizungumza
na Mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa wilaya hiyo Ernest Kahindi alisema kunyesha kwa mvua hizo kumesababisha
kuwepo kwa maji mengi yaliyokuwa yakitokea milimani na kuelekea kwenye makazi
ya watu.
Kahindi
alivitaja vijiji vilivyoathiriwa kutokana na maafa hayo ni Mbamba bay, Kilosa,
Ngindo, Lundo na kwamba mtu aliyefariki ni mkazi wa kijiji cha Ndengele anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 55, ambapo
alikutwa na mauti wakati akitokea mtoni kuchota maji na jina lake bado halijafahamika.
Vilevile
alieleza kuwa hali hiyo imesababisha ekari 45 za wananchi, zilizolimwa mazao ya
mihogo na mpunga zimesombwa na maji ikiwemo na skimu ya Kimbande ya kilimo cha
umwagiliaji zao la mpunga.
Katika
skimu hiyo mabanio mawili ya kuhifadhi maji kwa ajili ya shughuli za
umwagiliaji, yamebomoka na kusombwa na maji ikiwemo na mifereji yake ya
kupeleka maji shambani.
“Mifugo
iliyozolewa na maji na kufa ni ng’ombe tu, na sasa wamefikia idadi yake wapo
saba, hivyo tunaendelea kufanya tathimini na uchunguzi zaidi taarifa kamili ya
hata idadi nyumba zilizoathiriwa itatolewa baadaye”, alisema Kahindi.
Kadhalika
alisema madaraja manne yaliyojengwa katika vijiji vya Lipingo, Liuli, Lundo na
Ndengele yamezolewa na maji na kusababisha wananchi wanaoishi katika maeneo
hayo, kukosa mawasiliano kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Timu ya wataalamu ya wilaya ya Nyasa kwa kushirikiana na wilaya mama ya
Mbinga, wamekwenda huko kwa ajili ya kunusuru hali hiyo ikiwemo kuokoa na
kusaidia huduma muhimu kwa watu walioathirika.
Hadi sasa hali ya uokoaji inaendelea vizuri kutokana na maji kupungua,
lakini kumegundulika mnyama mkali aina ya mamba akizagaa nchi kavu katika eneo la Mbamba
bay mjini, ambapo timu ya wataalamu wa maliasili wamekwenda huko kwa ajili ya
kumuua ili asiweze kuleta madhara katika jamii.
No comments:
Post a Comment