Na Steven Augustino,
Tunduru.
MWANAFUNZI
anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Mwongozo kata ya Ligoma tarafa
ya Namasakata wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
ameumizwa vibaya katika mkono wake wa
kulia baada ya kukatwa na upanga na mwanafunzi mwenzake.
Ikra
Said mwenye umri wa miaka saba ndiye aliyekatwa mkono wake, na amelazwa katika
hospitali ya wilaya ya Tunduru akiendelea na matibabu.
Mwandishi
wa habari hizi amezungumza na majeruhi huyo ambapo alisema kuwa mkasa huo ulimpata wakati akiwa na
wanafunzi wenzake ambao walikuwa wametumwa na mwalimu waliye mtaja kwa jina
moja la Komba ili wakamtafutie kuni msitu uliojirani na shule hiyo.
Akifafanua
taarifa hiyo mwanafunzi huyo alisema kuwa wakati wakiwa katika harakati hizo za
kutafuta kuni, ghafla alijikuta akishambuliwa kwa kukatwa na panga katika mkono
wake wa kulia, na mwanafunzi mwenzake Ashraki Said anayesoma darasa la tatu
shuleni hapo.
Katika
taarifa hiyo mwanafunzi huyo baada ya kufanya tukio hilo, alikimbia na kumtelekeza katika eneo la
tukio kabla ya kuokolewa na wanafunzi wengine ambao walimpeleka nyumbani kwao,
na kuwaeleza wazazi wake juu ya mkasa huo.
Baba
mzazi wa majeruhi huyo Said Izulu alisema kuwa baada ya kumpokea mwanaye
aliyeumizwa alienda shuleni kwa ajili ya kutaka maelezo juu ya kilichotokea,
lakini hakupewa ushirikiano na walimu hali ambayo ilimfanya achukue jukumu la
kumkimbiza hospitali kwa ajili ya matibabu.
Alisema
kilicho msikitisha zaidi ni kitendo cha walimu hao akiwemo mwalimu ambaye
alitajwa kuwatuma watoto hao, ili wakamtafutie kuni kutoonesha ushirikiano
baada ya tukio hilo
baya kujitokeza.
Alipotafutwa
kaimu afisa elimu shule za msingi wilayani Tunduru, Flavian Nchimbi ili kuzungumzia
tukio hilo
hakupatikana ofisini kwake wala katika simu yake yenye namba 0755646719
haikuweza kupatikana.
Wakizungumza
kwa masharti ya kutotajwa majina yao
baadhi ya maofisa wa idara ya elimu wilayani humo, kwa madai kuwa wao siyo
wasemaji walisema kuwa endapo mwalimu Komba alichukua maamuzi ya kuwatumikisha
watoto kwa manufaa yake alifanya kosa.
Walisema
taratibu za kuwatuma wanafunzi kwenda kufanya kazi yoyote yenye manufaa ya
shule, hutakiwa kufanya kazi hizo mbele ya usimamizi wa mwalimu na kwamba hata kama kuni hizo walizokuwa wametumwa ni kwa ajili ya
kupikia chakula cha wanafunzi, ilitakiwa awepo mwalimu ili kuepusha matatizo
yanayoweza kutokea baadaye.
No comments:
Post a Comment