Tuesday, May 7, 2013

WASAUDI ARABIA MBARONI, WADAIWA KUHUSIKA NA TUKIO LA BOMU ARUSHA

                      Daktari wa Hospitali ya Mount Meru Jijini Arusha,      akimuhudumia mtoto aliyepigwa na bomu. 
Na Mwandishi wetu,

WAKATI Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, akikatisha ziara yake nchini Kuwait, kurudi hapa nchini kwa lengo la kuungana na Watanzania wenzake katika kipindi hiki kigumu, Jeshi la Polisi  linawashikilia watuhumiwa kadhaa kwa madai ya kuhusika na mlipuko wa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu, lililorushwa siku ya Jumapili katika Kanisa katoliki la Olasiti Jijini Arusha.
Miongoni mwa washukiwa ambao wako mikononi mwa polisi ni raia wanne wa Saudi Arabia na wengine wanne ni raia wa Tanzania. 


Wakati mwandishi wa BBC Baruan Muhuza akizungumza akiwa Hospitalini mjini Arusha alisema, idadi ya watu waliofariki dunia kufuatia mlipuko huo wanafikia kuwa ni wawili, na sio watatu kama ilivyoripotiwa hapo awali.

Katika hatua nyingine imethibitishwa kuwa watu wawili wamefariki dunia katika mlipuko huo uliotokea majira ya saa tano asubuhi katika kanisa hilo na wengine kadhaa kujeruhiwa huku balozi wa Papa na watawa waliokuwa katika shughuli hiyo maalum ya uzinduzi wa parokia hiyo mpya ya Mtakatifu Yosefu mfanyakazi wakinusurika pia.

Padri Festus Mangwangi ambaye ni Paroko msaidizi wa kanisa Katoliki jimbo la Arusha alisema mlipuko huo ulipotokea walikuwa  katika hatua ya kubariki maji kwa ajili ya uzinduzi wa kanisa hilo, uliokuwa ukiongozwa na balozi wa Papa Francis. 

Hili ni shambaulio la kwanza la bomu nchini Tanzania japo kuwa mwaka huu pia kulikuwa na mtukio ya mauaji ya Padre wa kanisa katoliki visiwani Zanzibar, Everest Mushi ambaye alipigwa risasi wakati akiwa anajiandaa kuingia Kanisani kwa ajili ya kuendesha ibada.

No comments: