Spika Anna Makinda akizungumza na Wabunge Dodoma leo. |
BUNGENI DODOMA:
HALI imekuwa tete
mkoani Mtwara kufuatia mapambano ya wananchi na askari wa Jeshi la Polisi
yakiendelea mkoani humo, ambapo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne
Makinda amelazimika kuahirisha vikao vya Bunge kwa siku ya pili sasa, ili kuipa
serikali nafasi ya kumaliza mgogoro huo ambao unaendelea.
Spika huyo alifikia
maamuzi hayo leo asubuhi baada ya Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dkt.
Emmanuel Nchimbi, kutoa maelezo ya serikali juu ya mapigano hayo yaliyoanza
jana mkoani humo.
Wananchi wa Mtwara
walianzisha mapigano hayo kwa lengo la kupinga hotuba ya Wizara ya nishati na madini,
iliyosomwa Bungeni na kuweka msisitizo kwamba gesi hiyo lazima isafirishwe hadi
Jijini Dar es Salaam.
Akiahirisha vikao
hivyo vya Bunge la bajeti Makinda alisema, endapo ataruhusu wabunge wajadili
maelezo ya serikali yaliyotolewa na Waziri Dkt. Nchimbi, hali hiyo itazidi
kuchochea mapigano hayo.
"Baada ya
kusikiliza maelezo ya serikali, naomba kuahirisha vikao vya bunge hadi kesho
saa tatu asubuhi, ili kutoa nafasi kwa kamati ya Bunge kukaa na kujadili suala hilo na kutafuta njia za
haraka za kuishauri serikali, badala ya
kuruhusu wabunge waanze kuchangia hoja za serikali na tayari nina wachangiaji
wengi hapa", alisema.
Akihutubia Bunge hilo kabla ya kuahirishwa Dkt. Nchimbi alisema "Kamwe serikali haiwezi kuwafumbia macho
wanasiasa wanaochochea vurugu hizi, watu wenye nia ya kuivuruga Tanzania, serikali
imeshajipanga namna ya kudhibiti hali hiyo na kuleta utulivu kwa wakazi wa
Mtwara", alisema Nchimbi.
Aliongeza kuwa "Katika
kuhakikisha kwamba hali hiyo inathibitiwa ipasavyo tayari askari 32 wa Jeshi la
Wananchi Tanzania(JWTZ) wamekwisha wasili mkoani Mtwara kutoka Nachingwea, kwa
ajili ya kusaidia Jeshi la Polisi, kuna askari wetu wanne waliokufa katika
ajali wakielekea Mtwara, hatuwezi kuacha damu zao zimwagike bure, kuna uharibifu
mkubwa wa mali ikiwemo nyumba ya Mwandishi wa habari wa shirika la utangazaji
Tanzania(TBC) pia imechomwa moto na kuteketea kabisa, haya yote hatuwezi
kuyavumilia", alisisitiza Nchimbi.
No comments:
Post a Comment