Freeman Mbowe. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALI ya kisiasa kwa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma
imeendelea kuwa tete, kufuatia viongozi wa chama hicho ngazi ya Wilaya na Jimbo
kuvuliwa madaraka, kutokana na kushindwa kukiimarisha chama na kutowajibika
ipasavyo.
Kauli hiyo ilitolewa na aliyekuwa Katibu wa Baraza la
vijana la chama hicho (BAVICHA) Felix Katoto, ambaye hivi sasa anashikilia
ofisi ya CHADEMA wilayani Mbinga kwa muda, kutokana na uongozi uliokuwa awali
kuondolewa madarakani.
Katoto alisema hayo alipokuwa akihojiwa na mwandishi
wa habari hizi ofisini kwake, ambapo alieleza pia uongozi huo wa awali ulikuwa
hautekelezi majukumu ya chama kwa mujibu wa taratibu walizojiwekea, na ndio
maana wamefikia maamuzi hayo.
“Tumefanya hivi tukiwa na malengo ya kukijenga chama
chetu, uongozi uliopita ulikuwa una matatizo ambayo hata yamesababisha chama
kushindwa katika chaguzi mbalimbali zilizofanyika ndani ya wilaya hii”,
alisema.
Alifafanua kuwa chaguzi hizo ni za nafasi ya diwani,
ambazo madiwani wa maeneo husika mmoja alifariki dunia wa kata ya Langiro na
mwingine aliyejiuzuru wa kata ya Mpepai ambapo wakati uchaguzi unafanyika
katika maeneo hayo, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Desderius Haulle na
viongozi wenzake, muda mwingi walikuwa wakizembea na hata wakati mwingine
kuonekana wakishiriki kukidondosha chama kisiweze kushinda katika chaguzi hizo
zilizofanyika hivi karibuni.
“Uwezo wa kushinda katika kata hizi tulikuwa nao kwa
kiasi kikubwa lakini hawa viongozi wenzangu ambao sasa hatupo madarakani,
walikuwa hawazingatii majukumu yao
waliyopewa kiasi ambacho hata fomu za wagombea wetu siku ya mwisho ya
kuzirejesha utakuta zinamapungufu”, alisema Katoto.
Aidha alitolea mfano kwa kata ya Langiro ambayo
uchaguzi umefanyika hivi karibuni, kwamba siku wanarejesha fomu ya mgombea wao
wa udiwani ilipopokelewa na msimamizi wa uchaguzi ilikuwa na mapungufu makubwa,
kama vile kutogongwa mihuri na kuwekwa sahihi na wahusika na hatimaye kushindwa
kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho hivyo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kufikia hatua ya kushinda bila kupingwa.
Kutokana na uzembe huo alisema wanachama wa CHADEMA
wilayani Mbinga, walikuwa wakiutupia lawama uongozi uliokuwa madarakani hivyo
baada ya malalamiko hayo kufikishwa katika ngazi husika, ndipo walipotakiwa
kuwajibika kuondoka madarakani na wakati wowote uchaguzi wa viongozi wengine
wapya utafanyika mara baada ya taratibu husika kukamilika.
Kadhalika alipoulizwa Mwenyekiti wa CHADEMA wa mkoa wa
Ruvuma, Joseph Fuime alithibitisha kwa uongozi wa chama hicho wilaya ya Mbinga
kuondolewa madarakani, huku akisema wakati uongozi huo unawajibika kutekeleza hilo yeye alishiriki kusimamia suala hilo.
Viongozi waliojiuzuru na wadhifa wao kwenye mabano
ngazi ya Wilaya ni Desderius Haulle (Mwenyekiti), Alfonce Nchimbi (Katibu),
Ferdinand Mbelle (Katibu Mwenezi), Gaudensia Komba (Mwenyekiti baraza la umoja
wa akina mama), Anastazia Magubika (Katibu wa baraza la umoja wa akina mama),
Menas Ndunguru (Mwenyekiti baraza la wazee), Nathaniel Ndunguru (Katibu baraza
la wazee), Dominicus Ngalima (Mwenyekiti baraza la vijana) na Felix Katoto
(Katibu baraza la vijana).
Wengine kwa ngazi ya Jimbo ni Winfrid Ndunguru
(Mwenyekiti), Pius Ndimbo (Katibu), Daud Mwalongo (Katibu mwenezi), Theopista
Haulle (Baraza la umoja wa akina mama), Magreth Swai (Katibu baraza la umoja wa
akina mama), Peter Ngunguta (Mwenyekiti baraza la wazee), Jacob Ndunguru
(Katibu baraza la wazee), Jacob Ngonyani (Mwenyekiti baraza la vijana) na
Stanley Ndunguru (Katibu baraza la vijana).
No comments:
Post a Comment