Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya viongozi Waandamizi wa wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, wamenyoshewa kidole na
kulalamikiwa kwamba, wamekuwa wakifumbia macho malumbano yanayoendelea
kushamiri katika idara ya elimu wilayani humo.
Aidha
vigogo hao wilayani humo, wametupiwa lawama kwamba wengine wamekuwa wakishiriki
katika kuendeleza malumbano hayo, na hata kufikia hatua ya kukatisha tamaa kwa
baadhi ya watendaji wa idara hiyo, ambao wanaonekana kufanya vizuri katika kukuza
maendeleo ya sekta hiyo ya elimu.
Kwa
ujumla hivi sasa kumekuwa na mgogoro mzito katika idara ya elimu wilayani
Mbinga, hasa kwa kitengo cha elimu ya msingi jambo ambalo linazua malalamiko
kutoka miongoni mwa wadau wa elimu.
Madai
hayo yalitolewa leo kwenye kikao cha tathimini ya Wadau wa elimu, kilichoketi kwenye ukumbi
wa Jimbo la Mbinga, Kanisa katoliki uliopo mjini hapa ambacho kilikuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wake, ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga.
Sambamba
na hilo Mwenyekiti wa huduma za jamii wilayani Mbinga James Yaparama,
alimnyoshea kidole Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga akisema tatizo hili lipo katika
ofisi yake na analifahamu, lakini inashangaza kuona mhusika anayeendeleza
mgogoro huo kutochukuliwa hatua za kisheria.
“Mheshimiwa
mkuu wa wilaya, kuna kigugumizi gani kilichopo ambacho mtu anayetuvuruga unamfahamu
na unashindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi yake?, tunaishia kuunda tume ya
kuchunguza tatizo hili na kumaliza hela za halmashauri kwa kulipana posho juu
ya jambo hili, wakati lipo wazi linajulikana”, alisema James Yaparama.
Naye
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Desderius
Haulle akichangia hoja katika kikao hicho, alimshushia shutuma nzito Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Mbinga Shaibu Nnunduma kwa
kile alichoeleza kuwa, ndiye kinara namba moja anayehusika katika
kuendeleza mgogoro huo huku akijua kwamba hilo ni kosa kwa mujibu wa
sheria za utumishi wa umma.
Desderius
Haulle baada ya kutamka hilo alimtaka Mkuu wa wilaya hiyo kuchukua
hatua mapema, kwa kulifanyia kazi huku akieleza kuwa habari zinazozungumzwa na wadau wa elimu katika
maeneo mbalimbali wilayani Mbinga, kwamba Mkurugenzi huyo wa halmashauri
ya wilaya hiyo kwa kiasi kikubwa amekuwa ndio chanzo cha mgogoro huo.
"Mheshimiwa
mkuu wa wilaya hiki ambacho kinafanywa na mkurugenzi huyu si cha
kukifumbia macho, ni vyema hatua sasa zichukuliwe kwa kulifanyia kazi
haraka", alisisitiza Desderius Haulle.
Diwani wa viti maalum Tarafa ya Mbinga mjini Grace Millinga aliendelea kupigilia msumali wa moto
akisema, katika kipindi cha miaka ya nyuma malumbano haya hayakuwepo lakini
watu wachache tu ndio wanaonekana kutaka kurudisha nyuma sekta ya elimu
wilayani humo, kwa maslahi yao
binafsi.
“Leo
hii malumbano haya yanafanywa na baadhi ya watumishi ambao si wazawa wa wilaya
hii, sisi tuna uchungu sana,
kwa niaba ya wenzangu tunasema hatutakubali kuvumilia hali hii iendelee
tunapoona wenzetu hawa wanaturudisha nyuma”, alisema Grace Millinga.
Diwani
huyo alieleza kuwa kundi hilo la watu wachache
kazi yao ni kupiga majungu tu, huku akiongeza mbele
ya mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga kwamba, kama
hali hiyo itaendelea kufumbiwa macho ipo siku yeye yupo tayari kulitaja jina la
mtu anayehusika katika malumbano hayo ya kurudisha nyuma sekta ya elimu
wilayani humo.
“Huyu
mtu mheshimiwa mkuu wa wilaya ofisi yako inamfahamu, unao uwezo wa hata
kumwajibisha kwa namna moja au nyingine ikiwemo hata kumhamisha akafanyie kazi
maeneo mengine, kwa nini usituondolee huyu mtu?”, alihoji Grace Millinga.
Kadhalika
Mratibu wa elimu kata ya Luwaita Laurent Nsuha alisema kumekuwa na barua
zinazoendelea kuandikwa na kumchafua ofisa elimu shule za msingi ambazo hazina
msingi wa aina yoyote ile, hali ambayo imekuwa ikikatisha tamaa na kurudisha
nyuma maendeleo ya sekta ya elimu wilayani Mbinga.
“Mheshimiwa
mkuu wa wilaya, ninyi viongozi waandamizi mnapaswa kutoa ushirikiano juu ya
tatizo hili kwa kulifanyia kazi haraka, na sasa nashauri hebu tukae na kuangalia
tunaendesha vipi mustakabali wa maendeleo ya elimu kwa shule zetu za msingi
hapa wilayani, inakuwa si vyema viongozi wachache kulumbana kwa maslahi binafsi,
lakini tunafahamu na ninyi viongozi waandamizi mpo katika mgogoro huu”, alisema
Laurent Nsuha.
Naye
Diwani wa kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda alisema mahusiano kwenye ofisi za
vigogo wa ngazi ya wilaya, sio mazuri hivyo wao kama
wadau wa elimu wanaona wanakoipeleka jamii hii ya wanambinga sio kuzuri,
kutokana na kuendeleza migogoro isiyokuwa ya lazima.
Kwa
upande wake mkuu wa wilaya ya Mbinga
Senyi Ngaga akijibu malalamiko hayo katika kikao hicho cha wadau wa elimu
alisema, “Ni kweli barua za migogoro juu ya tatizo hili ofisi yangu na kamati
yangu ya ulinzi na usalama tumeziona na tunaendelea kuzifanyia kazi”.
Senyi
Ngaga alifafanua kuwa ofisi yake imekwisha anza pia kukaa vikao na maofisa
husika kutoka idara ya elimu wilayani humo, hivyo anachohitaji zaidi ni
ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali, katika kumaliza mgogoro huo.
Wakizungumza
na Mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti na sharti la kutotajwa majina
yao katika mtandao huu, wadau hao wa elimu walisema kuwa mgogoro huo
unasababishwa na baadhi ya viongozi wenye uchu wa madaraka na tamaa ya fedha
ambazo ni malimbikizo ya walimu ya likizo na uhamisho kwa shule za msingi, ambao
wamekuwa na tabia ya huko katika miaka ya nyuma wakizichota na kuzitumia kinyume
na taratibu kwa maslahi yao binafsi.
Walifafanua
kuwa kutokana na afisa elimu wa shule za msingi wilayani Mbinga, Daud Mathias
Mkali kujenga msimamo wake wa matumizi
mazuri ya fedha hizo na kuhakikisha walimu wanalipwa stahiki zao ipasavyo na
kwa wakati, ndio maana kunazua malumbano na kuandikiana barua za hapa na pale kwa
lengo la kutaka kumchafua ili hatimaye serikali au uongozi husika ufanye
taratibu za kuweza kumhamisha na kumpangia kituo kingine cha kufanyia kazi, ili
wao waweze kupata mwanya wa kupanga safu ya kumweka madarakani ofisa elimu
wanayemtaka wao na hatimaye wafanikiwe kuchota fedha hizo kama walivyozoea
katika miaka hiyo ya nyuma.
Hata
hivyo, miaka mitano iliyopita wilaya ya Mbinga kwa upande wa ufaulu wa elimu ya
msingi hali ilikuwa tete na sasa baada ya serikali kufanya utaratibu wa kuleta
ofisa elimu mwingine, mabadiliko katika sekta hii muhimu yamejitokeza na sasa
wilaya ya Mbinga imekuwa ikishika nafasi ya tatu kimkoa tofauti na miaka kadhaa
ya nyuma ilikuwa ikishika mkia.
No comments:
Post a Comment