Baadhi ya abiria wakiwa wamepanda gari ya mizigo mjini Iringa, kwa lengo la kuwahi katika maeneo yao ya kazi leo, baada ya madereva wa daladala kugoma kusafirisha abiria. |
Na Mwandishi wetu,
Iringa.
KWA siku ya leo kadhia za hapa na pale zimeanza kujitokeza katika mji wa Iringa, mkoani Iringa kufuatia mgomo wa daladala ambao umeanza kwa kasi na kuchukua sura mpya, hali ambayo imesababisha wananchi, kutembea kwa mguu umbali mrefu wakielekea katika maeneo yao ya kufanyia kazi.
Mgomo wa daladala umeanza kwa kasi katika mji wa Iringa baada ya daladala zote kugoma kufanya kazi, huku wanafunzi na wafanyakazi wa iadara mbalimbali wakichelewa kwenda katika vituo vyao vya kazi.
Hali hiyo ya mgomo imeanza kutikisa na kufanya polisi kuingilia kati kuwatuliza madereva wasigome jitihada ambazo zinaendelea hadi sasa.
Mwandishi wetu ambaye yupo katika maeneo mbalimbali ya mji huu, ameshuhudia hali jinsi ilivyo ambapo watu wanalazimika kupanda hata magari ya kubebea mizigo, ili waweze kufika katika vituo vyao vya kazi.
Machungu ya mgomo huu kwa kiasi kikubwa yameathiri maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa, ambapo usafiri ambao umeonekana ukifanya kazi sasa ya kusafirisha abiria ni bajaji, pikipiki na taxi huku nauli kwa mtu mmoja katika bajaji shilingi 3000 wakati taxi kwa kila kichwa shilingi 1000 hali ambayo wananchi wengi wenye kipato cha chini wanaonekana kushindwa kumudu gharama hizo.
Hadi habari hizi zinaenda mitamboni chanzo cha mgomo huo kinatokana na madereva wa daladala katika mji huo kuzuiwa kuchukua abiria katika kituo kimoja kilichopo mjini hapa, badala yake wanaruhusiwa kushusha abiria tu na sio vinginevyo.
Vilevile baadhi ya abiria walikuwa wakiwalalamikia madereva hao kwamba, wamekuwa wakitoza fedha mara mbili endapo anatoka kituo kimoja kwenda kingine, jambo ambalo limesababisha adha hiyo kujitokeza.
No comments:
Post a Comment