Askofu Norbeth Mtega. |
Na
Mwandishi Maalum,
Songea.
ASKOFU Mkuu wa
Kanisa Katoriki, Jimbo Kuu la Songea, mkoani Ruvuma ambaye juzi ametangaza
kujiuzulu, Norbert Mtega, ameelezea sababu zilizomfanya achukue uamuzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema
hali hiyo inatokana na kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali ambayo ni presha,
miguu, magoti kujaa maji na kukosa usingizi kwa muda mrefu hivyo kujisikia
kizunguzungu na tayari amewahi kuanguka zaidi ya mara nne.
Alisema jamii inayomtazama inamuona yupo kawaida
lakini ana matatizo makubwa ya kiafya kwa muda mrefu ila alikuwa akijitahidi
kufanya kazi za kitume hali ambayo imechangia afya yake kuendelea
Aliongeza kuwa, tatizo la afya yake ni la muda
mrefu hivyo ni bora astaafu mapema kabla ya kupoteza kumbukumbu ili aweze kumpa
Baba Mtakatifu muda wa kutafuta Askofu mwingine ambaye ataweza kuongoza jimbo hilo.
“Nimeamua kujiuzulu kwa manufaa ya Wakatoliki
wote, Jimbo Kuu la Songea na jamii kwa ujumla ili niweze kupatiwa matibabu
kwani nikiendelea kung’ang’ania uongozi, hasara yake ni kubwa sana kwa jamii ninayoiongoza.
“Namuomba Mungu anipe afya njema ili niweze
kutoa ushauri zaidi kwa waumini, Mapadri na Serikali,” alisema.
Amewahimiza waumini na viongozi wa dini,
kuendelea kuwa na ushirikiano, kuacha tofauti za ukabila ambazo zinachangia
kurudisha nyuma maendeleo ya Mkoa huo kwani ukabila ni hatari na unaweza
kuwagawa, kukwamisha maendeleo.
Alisema yeye anatambua kuwa, watu wengi
wameshtuka kutokana na uamuzi aliochukua hasa kwa kuzingatia kuwa, alikuwa
akifanya kazi zake bila wasiwasi.
Amemtaka Askofu ajaye, kuhakikisha anaendeleza
mema aliyoanzisha hususani katika nyanja ya elimu, afya, maji, mazingira ili
kuwaletea wananchi maendeleo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano na ushauri.
Mkazi wa Mkoa huo, Watson Nganiwa, alisema Mtega
atakumbukwa kutokana na kuwajengea uwezo wananchi wajitegemee na kuacha kutegemea wafadhili, kuhimiza wafanye kazi kwa bidii si kutegemea
misaada.
Alikuwa
akishiriki shughuli mbalimbali za kijamii, kiserikali na kuwashirikisha
viongozi wa Serikali pamoja na kukemea maovu miongoni mwa jamii bila woga.
Wananchi wengi wamempongeza kwa
uamuzi aliochukua na kumtakia afya njema ili aweze kupona, kuendelea kutoa
ushauri na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wake.
Mtega amelitumikia Jimbo la Iringa kwa miaka
sita na baadaye Jimbo la Songea miaka 22 hivyo amekuwa askofu kwa muda wa miaka
28, Kiongozi wa Idara ya Elimu katika Baraza Kuu la Maaskofu na Msimamizi wa
kitume katika majimbo nane.
No comments:
Post a Comment