Na
Steven Augustino,
Tunduru.
MADIWANI
wameiomba Serikali kuwabana baadhi ya walimu wa shule za Msingi na Sekondari,
wanaoendesha miradi ya kuonesha picha za video katika maeneo ya shule, huku
wakieleza kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya maendeleo ya elimu kwa watoto wao.
Hayo
yalisemwa na diwani wa viti maalum katika kata ya Nalasi Alus Yunusi, ambaye
alisema kutokana na hali hiyo walimu hao wamekuwa hawazingatii maendeleo ya
taaluma kwa wanafunzi, zaidi ya kuangalia maslahi yao yatokanayo na miradi hiyo.
Akifafaa
taarifa hiyo Yunusi alisema kuwa hayo ameyabaini katika tarafa yake, ambapo
biashara hiyo ya kuonyesha picha za video imekithiri na kwamba endapo watafumbiwa
macho taaluma katika wilaya hiyo itaendelea kuporomoka.
Kufuatia
hali hiyo Diwani huyo akatumia nafasi hiyo kuwakumbusha wakaguzi wa shule,
kutazama changamoto hiyo na kuweka mikakati ya kuidhibiti na ikiwezekana
biashara hiyo izuiliwe kufanyika katika maeneo ya shule.
Alisema
kutokana na hali hiyo walimu hao wamekuwa hawawezi kuwakemea wanafunzi hao,
hata wakifanya matukio mabaya kwa vile wao ndio wateja wakubwa wa kuangalia picha
za video.
Diwani
wa kata ya Masonya Fadhili Mshamu na diwani wa viti maalumu katika tarafa
ya Nampungu Sikudhani Chikambo, walieleza kilio cha ukosefu wa nyumba za
walimu katika shule za wilaya ya Tunduru, huku wakisisitiza ni vyema iwekwe mikakati ya kumaliza tatizo hilo ili
walimu waondokane na adha ya kupanga uswahilini.
Diwani
Chikambo katika taarifa yake pia alieleza kilio cha utoro wa kupindukia
katika shule ya msingi Mchekeni, ambapo alisema kuwa hivi sasa kuna darasa moja
wanasoma wanafunzi wawili tu, hali ambayo alisema inahitaji mikakati ya
makusudi kuwaokoa watoto wao kwa kuwafanya wapende masomo.
Aidha
taarifa ya madiwani hao pia ikabainisha ubovu wa miundo mbinu ya shule pamoja
na uchakavu wa madarasa katika shule nyingi wilayani humo, kutokana na kuta zake kubomoka.
Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Robert Nehatta alisema kuwa, halmashauri
yake imejipanga kuhakikisha kuwa inaboresha miundombinu katika maeneo ya kazi, ikiwemo
ujenzi wa nyumba za walimu na miradi mingine ya maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment