Thursday, May 23, 2013

HALI YAZIDI KUWA TETE MKOANI MTWARA, WATU 91 WATIWA MBARONI

Jinsi hali ilivyokuwa tete mkoani Mtwara.














MTWARA, TANZANIA:

Waziri wa mambo ya ndani Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa tamko kali hivi karibuni juu ya  vurugu zinazoendelea kutokea katika Manispaa ya Mtwara, kwamba damu ya Wanajeshi wanne waliofariki katika ajali haitamwagika bure, na kwamba vyombo vya usalama vinawasaka ndani na nje ya nchi watu wote wanaohusika na vurugu hizo.
Askari waliopoteza maisha ni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao walipata ajali wakati wakitoka Nachingwea kwenda Mtwara, ili kuongeza nguvu katika kutuliza ghasia.

Dk Nchimbi amesema wanajeshi 32 waliagizwa kwenda kuongeza nguvu na kwamba waliojeruhiwa ni katika  ajali hiyo 20.


Katika vurugu za jana mtu mmoja ameripotiwa kufariki dunia. Mganga mkuu wa hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dkt. Mohamed Kodi alisema maiti moja imepokelewa katika hospitali hiyo.

Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo bungeni kwa niaba ya Waziri mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa asome tamko la serikali kuhusu vurugu za Mtwara.

WATU 91 WATIWA MBARONI:


Akitoa tamko hilo Dkt. Nchimbi alisema tayari watu 91 wametiwa mbaroni kwa madai ya kuhusika kuharibu miundombinu na kuchoma moto nyumba.

Waziri huyo ameliambia Bunge kwamba kundi la vijana  limechoma moto nyumba ya mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), Kassim Mikongolo, nyumba ya mbunge wa Mtwara mjini (CCM) Hasnein Murji na Waziri wa nchi,  Ofisi ya Waziri mkuu, (TAMISEMI) ambaye pia ni mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia zimeteketezwa kwa moto.

Vilevile ofisi ya CCM ya kata na ofisi ya serikali ya kata zilizoko mtaa wa Majengo zimechomwa moto na kundi la vijana, ikiwamo pia nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mtwara Mikindani,  Ali Chinkawene  kurushiwa mawe.

Ofisi ya Mtendaji mtaa wa Msikitini, kata ya Reli na ofisi ya CCM Chikongola nazo zimeteketezwa kwa moto.


Wakati hayo yakitokea wanafunzi wa shule za msingi Shangani na Majengo walirejeshwa  nyumbani, baada ya mabomu ya machozi kurindima kuanzia asubuhi  hadi mchana.
Mbali na hayo Dkt. Nchimbi ameonya watu wanaotaka rasilimali zitumike katika eneo zinakopatikana kwa kuwa tabia hiyo italipasua Taifa vipande vipande.

Alisisitiza kuwa vyombo ya usalama vitawasaka wahusika ndani na nje ya nchi ili kukomesha tabia hiyo.

 

No comments: