Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAKAZI
wa kijiji cha Tinginya tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
wameipongeza serikali kwa kuwafungia mfumo wa umeme Jua(SOLA) katika zahanati yao na kueleza kuwa mradi
huo, utawakomboa wanawake ambao kwa muda mrefu walikuwa wakijifungua wakiwa
gizani.
Fatuma
Mapila na Alihad Abdalahman ambao walikuwa wamepeleka mtoto wao kwa ajili ya
matibabu na muuguzi wa zahanati hiyo, Grolia Lupindo ni miongoni mwa baadhi ya wananchi
ambao walishindwa kuzuia furaha yao, baada ya kushuhudia wakati mfumo huo
ukiwashwa katika zahanati yao na katika nyumba ya mganga, iliyopo jirani na
eneo hilo la kutolea huduma ya afya.
Wakizungumza
kufuatia hali hiyo walisema, kwa muda mrefu tangu zahanati yao ifunguliwe
mwaka 1990 na kuanza kutoa huduma, wanawake wa kijiji cha Tinginya na vitongoji
jirani walikuwa wakitumia vijinga vya moto kumulikia wakati wa kujifungua, hali
ambayo ilikuwa ikihatarisha maisha yao na watoto wanaojifungua.
Awali
akizungumza na wananchi hao afisa mafunzo na ujengaji wa uwezo kutoka wakala wa
nishati Vijijini(REA) Mary Ngusaru alisema, ufungaji huo wa mfumo wa umeme jua
umefanywa na vijana 35 waliomaliza mafunzo ya siku 7 na kwamba hivi sasa wilaya
ya Tunduru, imepata hazina ya mafundi wenye uwezo wa kufunga mfumo huo na
kufanya matengenezo madogo mdogo wakati kunapotokea
hitilafu.
Ngusaru
alifafanua kuwa hadi kukamilika kufungwa kwa mfumo huo na mfumo mwingine
utakaofungwa katika zahanati ya kijiji cha Nampungu, utagharimu jumla ya
shilingi milioni 20 ambazo zimetolewa na serikali kupitia mpango wa changamoto
za milenia (MCC).
Naye
mwezeshaji wa mafunzo hayo mhandisi Philbert Beyanga kutoka kampuni
ya Solar Energy alisema, katika kipindi hicho vijana hao wamenolewa na kupatiwa
ujuzi huo ikiwemo uendelezaji wa teknolojia ya umeme jua, nishati upepo, na
nishati ya maporomoko ya maji.
Alisema
mfumo wa umeme jua katika zahanati ya kijiji hicho ambao umejengwa, unao uwezo
wa kuwasha taa 36 pamoja kumudu kuendesha mashine za kupimia ugonjwa wa Malaria,
jambo ambalo litarahisisha utendaji wa kazi kwa watumishi wa zahanati hiyo.
No comments:
Post a Comment