Matrekta yakifanya kazi ya kuchimba mkaa wa mawe katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said
Mwambungu, amelazimika kuufunga kwa muda
usiojulikana, mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro
kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoani humo, baada ya wananchi wa kijiji hicho kumtaka
mkuu huyo wa mkoa aufunge mgodi huo mpaka watakapolipwa madai yao ya muda mrefu
ya fidia wanazodai, pamoja na kuyaweka mazingira yao katika hali inayostahili
kwa matumizi ya binadamu.
Mradi huo wa makaa ya mawe
unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa
zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC, na
asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.
Mwambungu alichukua uamuzi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye uwanja wa shule ya msingi Ntunduaro, ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa
wa wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ngazi
ya wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma, pamoja na viongozi wa vyama vya
siasa.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alimkaribisha mkuu wa
mkoa huo Mwambungu, ili azungumze na wananchi kuhusu mgogoro uliopo kati ya
wananchi na mwekezaji wa mgodi huo.
Baada ya kukaribishwa mkuu huyo wa mkoa alianza kwa kusema
“wananchi wa Ntunduaro hoyee! wananchi wakajibu hoiiii! huku wakipaza sauti
zao, mpaka kieleweke”.
Kwa ujumla hali ilikuwa tete ambapo Mwambungu
aliwataka wananchi hao kuwa watulivu, wakati anapotaka kuwaambia nini
serikali yao imefanya katika kumaliza tatizo hilo.
Pamoja na mkuu huyo wa mkoa kujaribu kuwatuliza wananchi
hao, bado hali iliendelea kuwa mbaya baada ya wananchi kumshinikiza Mwambungu waende nae mpaka kwenye eneo la mgodi
akaufunge na kama haitawezekana basi wapo tayari kufa kwa kupigwa risasi kuliko
kufa kwa njaa wakati haki zao zipo na zinadhulumiwa na watu wachache.
Wananchi hao walisema matatizo na dhuluma iliyopo
yanasababishwa na viongozi wa serikali huku baadhi yao wakiugua magonjwa mbalimbali kutokana na kunywa maji yenye chembechembe ya sumu ya
madini ya makaa ya mawe yanayochimbwa eneo la kijiji hicho.
Mto Nyamabeva uliopo katika kijiji hicho ambao ndio
tegemeo kubwa, maji yake yamechafuliwa na wawekezaji hao kutokana na mkaa wa
mawe.
Akitoa kero mbele ya mkuu wa mkoa mwananchi Erick
Mapunda alisema kuwa wamechoka na ahadi hewa za mwekezaji wa mgodi huo, ambazo
kila kukicha imekuwa ni siasa hivyo ujio wa mkuu huyo wa mkoa uwe ni hitimisho
la kwenda kuufunga mgodi, mpaka hapo watakapotimiziwa ahadi walizoahidiwa
pamoja na kuwalipa fidia wanazoidai kampuni ya Tancoal Energy.
Naye Joseph Messa alieleza kuwa yeye akiwa ni mwananchi wa
kijiji hicho, amekata tamaa ya maisha kwa sababu hali ya kijiji chao ni mbaya kwa
sasa, kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu ya barabara, maji, shule pamoja
na zahanati kwani watoto wao wamekumbwa na magonjwa ya kichocho ambayo hawajui
yanasababishwa na nini na kwamba wamekuwa wakinywa maji ya sumu tangu mgodi huo
uanze kufanya kazi, licha ya kuwa malalamiko hayo walikwisha yafikisha kwa viongozi
wa serikali ya kijiji, wilaya na mkoa.
Alisema inasikitisha kuona viongozi hasa ngazi ya wilaya
walikuwa wakionekana mara kwa mara kutembelea eneo la mgodi, na alidai kuwa
yawezekana wamejenga urafiki mkubwa na mwekezaji wa mgodi huo na ndio maana
kero zao zilikuwa hazifanyiwi kazi.
Kwa upande wake Benedina Komba alisema kuwa tangu
mgodi huo uanze kufanya kazi wananchi wa kitongoji cha Nkaya, walipewa ahadi ya
kuhama maeneo yao kwa muda kwa madai kuwa wataonyeshwa maeneo mengine ambayo
wangepewa fidia ili wakajenge nyumba za kuishi, jambo ambalo mpaka sasa halijatekelezwa na
hivi sasa wamebaki wakihangaika na watoto wao kutokana na njaa kwa kuwa eneo
walilokuwa wakilima mazao mbalimbali limechukuliwa na kampuni hiyo inayochimba
makaa ya mawe.
Wosteri Mapunda alielekeza shutuma nzito kwa waandishi wa
habari wa mkoa wa Ruvuma kwa kutoandika habari za mgogoro huo, tofauti na
waandishi wa mkoa wa Arusha ambao wamekuwa wakiandika habari za mgogoro wa
Loliondo, ambapo serikali baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari ilihamia huko,
ili kumaliza mgogoro uliopo na kwa nini Ntunduaro ishindikane kwa muda wa miaka
mitatu sasa.
Aidha Johoni Nyimbo alimnyooshea kidole Mbunge wa jimbo
la mbinga mashariki Gaudence Kayombo na kumkumbusha ahadi aliyowaahidi
wananchi wa kijiji hicho, Mei 19 mwaka 2011 kwenye mkutano wa hadhara kuwa
endapo wanakijiji hao hawatalipwa fidia wanazodai atajiuzuru nafasi aliyonayo
ya Ubunge, na kumtaka ajiuzuru nafasi hiyo mara moja jambo ambalo lilimpandisha
hasira na baada ya kauli iyo alilazimika kusimama ili kutoa ufafanuzi wa
kauli yake hali ambayo ilisababisha kuwapandisha hasira wananchi hao na kuanza
kumzomea.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa
Ruvuma, Oddo Mwisho naye alikumbwa na adha ya kuzomewa baada ya kusimama na kuanza kujieleza kuhusiana na
jitihada za chama cha mapinduzi na serikali yake ya wilaya na mkoa huo, kwamba kwa
muda mrefu wamekuwa wakifanya mazungumzo kupitia Wizara ya nishati na madini,
Shirika la maendeleo la Taifa(NDC) pamoja na mwekezaji wa kampuni ya Tancoal
Energy, kwa lengo la kumaliza mgogoro uliopo kati ya mwekezaji na wananchi.
Kufuatia vurugu zilizojitokeza kwenye mkutano huo mkuu wa
mkoa Mwambungu alilazimika kusitisha mkutano huo kwa muda na kuwataka
wananchi hao warudi eneo la mkutano baada ya nusu saa, ili apate nafasi ya
kujadiliana na kamati yake ya ulinzi na usalama na baadae baada ya nusu saa
kupita, mkutano ulianza ambapo mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, aliwaeleza wananchi
hao kuwa amesikia maoni yao na amefikia hatua ya kuufunga mgodi huo kwa muda usiojulikana
hadi hapo madai yao ya msingi yatakapofanyiwa kazi na kutekelezwa.
Kwa ujumla mgogoro uliopo kati ya mwekezaji wa mgodi huo
na wananchi wa kijiji cha Ntunduaro unatokana na kampuni ya Tancoal Energy
kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya ukarabati wa zahanati ya
kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji, shule na ulipaji wa fidia kwa wananchi
306 ambao wamefanyiwa tathimini.
Pia madai mengine ni kwamba zaidi ya wananchi 400 ambao
awali walilipwa fidia zao, ilionekana fedha walizolipwa ni kidogo hivyo nao
walipewa ahadi ya kuongezewa malipo mengine, jambo ambalo hadi leo hii
halijatekelezwa.
|
No comments:
Post a Comment