Mtambo maalum, ukifanya kazi ya kuchimba makaa ya mawe huko kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi
Mbinga.
MGODI wa makaa ya mawe Ngaka
uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma ambao ulifungwa kwa muda usiojulikana sasa
umefunguliwa rasmi, na mwekezaji husika ameruhusiwa kuendelea na shughuli za
uchimbaji wa makaa hayo.
Ufunguzi huo umefanyika hivi
karibuni Mei 3 mwaka huu majira ya mchana na mkuu wa mkoa wa Ruvuma
Said Mwambungu, ambaye ndiye aliyeufunga Aprili 30 mwaka huu.
Mwambungu alitoa kauli ya kuufungua
mgodi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa eneo la ofisi
za kijiji cha Ntunduaro, ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa
kijiji hicho, wakiwemo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya
ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.
Akihutubia katika mkutano huo,
mkuu huyo wa mkoa alisema uamuzi wa kufungua mgodi wa makaa ya mawe Ngaka
umetokana na makubaliano yaliyofanyika na mwekezaji wa mgodi huo, kwamba katika
kipindi cha siku 45 kuanzia Mei 4 mwaka huu, mwekezaji husika anatakiwa
kukamilisha kazi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama na kuisambaza
katika makazi ya wananchi wa kijiji hicho.
Aidha juu ya madai ya fidia ya
wananchi hao, mwekezaji pia amepewa siku 45 kuhakikisha kila mtu anayedai awe
amelipwa na mwisho wa malipo ni June 15 mwaka huu.
Licha ya mkuu huyo wa mkoa kutoa
tamko hilo la kuufungua mgodi, baadhi ya kundi
la wananchi lilionekana kupinga wakidai usifunguliwe hadi madai yao ya msingi
yatakapotekelezwa, lakini Mwambungu na kamati yake ya ulinzi na usalama
aliyoongozana nayo waliendelea kuwasihi wananchi hao na ndipo walipofikia
uamuzi wa makubaliano kwamba ufunguliwe.
Awali kufungwa kwa mgodi huo wa
makaa ya mawe kulitokana na wananchi wa kijiji cha Ntunduaro, kumtaka mkuu huyo
wa mkoa aufunge mpaka watakapolipwa madai yao ya muda mrefu ya fidia wanazodai,
pamoja na kuyaweka mazingira yao katika hali inayostahili kwa matumizi ya
binadamu.
Mradi huo wa makaa ya mawe
unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa
zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC, na
asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.
Kwa ujumla siku ambayo mkuu huyo
wa mkoa alichukua uamuzi wa kuufunga mgodi huo, hali ilikuwa tete ambapo
wananchi walikuwa wakipiga kelele na kutoa vitisho wapo tayari hata kufa kwa
kupigwa risasi endapo madai yao
ya msingi hayatatekelezwa, na haki zao zipo na zinadhulumiwa na watu wachache.
Wananchi hao walikuwa wakipaza
sauti zao wakisema matatizo na dhuluma iliyopo yanasababishwa na viongozi wa
serikali, huku baadhi ya wananchi wakiteseka na kuugua magonjwa mbalimbali
kutokana na kunywa maji yenye chembechembe ya sumu ya madini ya makaa ya
mawe, yanayochimbwa katika eneo la kijiji hicho.
Mto Nyamabeva uliopo katika kijiji
hicho ambao ndio tegemeo kubwa, maji yake yamechafuliwa na wawekezaji hao kutokana
na vumbi la mkaa wa mawe.
Kwa ujumla mgogoro uliopo kati ya
mwekezaji wa mgodi huo na wananchi wa kijiji cha Ntunduaro unatokana pia na
kampuni hiyo ya Tancoal Energy kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya
ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji, shule na
ulipaji wa fidia kwa wananchi 306 ambao wamefanyiwa tathimini.
Hata hivyo madai mengine ni kwamba
zaidi ya wananchi 400 ambao awali walilipwa fidia zao, ilionekana fedha
walizolipwa ni kidogo hivyo nao walipewa ahadi ya kuongezewa malipo mengine,
jambo ambalo hadi leo hii halijatekelezwa.
No comments:
Post a Comment