Dar
es Salaam,
Tanzania.
MDHIBITI
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) ameanza ukaguzi maalumu katika
Halmashauri ya Bukoba Mjini kuhusu ubadhirifu wa fedha mbalimbali za miradi ya
maendeleo zilizokuwa zinatumika kwenye halmashauri hiyo.
Uamuzi
wa CAG umekuja baada ya Kamati Kuu ya CCM kumtaka CAG kufanya ukaguzi katika
halmashauri hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa za ubadhirifu wa fedha za miradi
ya maendeleo zinazodaiwa kuidhinishwa na Meya wa Halmashauri hiyo, Anatory
Aman.
Miradi
hiyo ni pamoja na mradi wa upimaji wa viwanja vya Mji wa Bukoba, ukarabati wa
soko na ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ambayo inadaiwa kuwa na harufu ya
ufisadi.
Akizungumza
na gazeti hili Dar es Salaam jana, Msaidizi wa CAG, Fransic Mwakapalila alisema
ukaguzi huo utaanza mwezi huu, ambao utahusisha kukagua miradi mbalimbali
iliyoainishwa kwenye hadidu za rejea.
Alisema
kutokana na hali hiyo, wakaguzi watafika kwenye halmashauri hiyo mwisho wa
mwezi huu kwa ajili ya kufanya ukaguzi huo.
“Tayari
tumepewa hadidu za rejea kwa ajili ya kufanya ukaguzi maalumu wa Halmashauri ya
Bukoba mjini, hivyo basi wakaguzi watafika katika halmashauri hiyo mwisho wa
mwezi huu,” alisema Mwakapalila.
Aliongeza
kuwa kutokana na hali hiyo, muda wa kukamilika kwa ukaguzi huo utatokana na
kukamilisha kwa shughuli hiyo, jambo ambalo linaweza kubaini ukweli kuhusu
uhalali wa matumizi ya fedha hizo au la.
No comments:
Post a Comment