Na Steven Augustino,
Tunduru.
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru
mkoani Ruvuma, limepitisha mapendekezo ya uundwaji wa mji mdogo, mgawanyo wa
eneo la utawala na kuridhia kuundwa kwa mkoa mpya utakaoziunganisha wilaya ya
hiyo na Namtumbo.
Mapendekezo hayo yalipitishwa katika kikao maalum kilichoketi
kwenye ukumbi wa Klasta mjini humo, na kwamba Madiwani hao walifikia
makubaliano hayo baada ya majadiliano ya muda mrefu ambapo awali, baadhi
yao walipendekeza uwepo wa mgawanyiko wa Wilaya mbili wakilenga kusogeza huduma
na kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo ambayo yalionekana kutoendana
na mapendekezo ya wataalamu ambao walienda na mapendekezo ya mgawanyo wa wilaya
mbili, Wilaya ya kwanza walitaka iundwe na tarafa za Matemanga na Nampungu wilaya
ya pili iundwe na tarafa za Nakapanya, Mlingoti na Namasakata na wilaya ya
tatu nayo ikitajwa kuundwa na tarafa za Nalasi na Lukumbule.
Akifafanua maelezo ya mgawanyo huo Diwani wa kata ya Ligunga
Kazembe Said alisema kuwa, kutakuwa na faida mbalimbali kwani katika kupatikana
kwa wilaya hizo tatu kutapanua huduma na kuiwezesha serikali kufikisha huduma
kwa wananchi wake kwa haraka, na kuyafikia malengo husika iliyojipangia kuwafikia
wananchi wake ifikapo 2020 na kwamba endapo watapendekeza mgawanyo
wa wilaya mbili watakuwa wameshiriki kulitenga eneo kubwa ambalo bado
litakuwa halifikiwi wa uirahisi kiutawala.
Uchache wa vigezo vilivyodaiwa kutakiwa kuangaliwa upya wakati wa mgawanyo huo, Diwani wa kata ya Masonya Fadhili Msahamu alisema
kuwa wilaya ya Namtumbo wakati inatangazwa kuwa Boma, wilaya yao ilikuwa na
tarafa 3, kata 13 na sasa inaomba kupewa wilaya ya pili ikiwa na wanazo
kata na kwamba wilaya ya Tunduru kwa sasa inazo kata 35, Tarafa 7 na
Vijiji 148 na eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 18,778 ambalo pia
linaweza kugawanywa na kuongeza maeneo ya utawala.
Upande wa uundaji wa mkoa mpya wa SELOU unaotarajiwa
kuunganisha wilaya za Tunduru na Namtumbo, Madiwani hao walipitisha bila mabadiliko
yoyote huku mgawanyo wa mapendekezo ya kuundwa kwa mamlaka ya mji mdogo wa
Tunduru, madiwani wa kata za Kidodoma Seif Miwani, Said Mkandu na Mbunge wa
jimbo la Tunduru Kusini Alhaji Mtutura walitoa mapendekezo ya kuongeza maeneo
mapya ili kuwa na eneo la kutosha.
Awali akitoa taarifa za mapendekezo hayo afisa mipango wa halmashauri
ya wilaya ya Tunduru, Kenneth Haulle aliwaeleza madiwani hao kuwa vigezo walivyopewa
kutoka ofisi ya Waziri mkuu ni pamoja na kuzingatia maeneo mbali mbali ikiwemo kigezo cha kwanza ni matumizi ya
takwimu mbali mbali ikiwemo zinazozungumzia idadi ya watu, vijiji, kata na
tarafa zilizopo wilayani humo.
Haulle aliendelea kufafanua kuwa wilaya ya Tunduru sasa inayo
majimbo mawili ya uchaguzi ya Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini yenye wakazi
298,274 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, inazo tarafa 7, kata
35, vijiji 148 na vitongoji 1,015 hali ambayo iliwasukuma wataalamu hao
kupeleka mapendekezo hayo ya mgawanyo wa wilaya mbili za kiutawala, wakiwa
wanafuata vigezo na maelekezo ya kitaifa yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa
mgawanyo huo.
No comments:
Post a Comment