Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
MADIWANI na watendaji katika halmashauri hapa nchini,
wametakiwa kujenga uwajibikaji na uwazi katika shughuli mbalimbali za maendeleo
ya wananchi, ili kuweza kuleta ufanisi na kukuza uelewa katika jamii.
Aidha kwa upande wa Madiwani wamesisitizwa kufanya mikutano na wananchi wao mara
moja kwa kila mwezi na kutoa elimu juu ya haki za binadamu, hususani kwa
wananchi walioachwa nyuma katika nyanja mbalimbali.
Rai hiyo imetolewa na Rosemary Manase, Wakili wa kituo cha Sheria
na Haki za binadamu hapa nchini, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari juu ya malengo mahususi ya mafunzo ya siku tatu ya haki za binadamu, yanayotolewa
na kituo hicho katika wilaya ya Nyasa na Mbinga mkoani Ruvuma.
Manase alisema mafunzo hayo yameshirikisha Madiwani na Watendaji
wa halmashauri za wilaya hizo, lengo hasa ikiwa ni kukuza uelewa wa sheria na
haki za binadamu kwa jamii, uwajibikaji na uwazi katika shughuli za halmashauri.
“Vitu vyote tunavyo wafundisha hawa wenzetu, tunahitaji
wavifikishe kwa wananchi, ni vizuri Madiwani wakayafikisha huko katika maeneo
yao ya kazi”, alisisitiza.
Aidha alifafanua kuwa wamekuwa wakielimisha juu ya masuala ya
rasimu ya katiba mpya, ambapo wamekuwa wakisisitiza juu ya wao
kupendekeza uwepo wa serikali moja
katika katiba ijayo.
“Sisi kwa upande wa kituo cha haki za binadamu, tunapendekeza
uwepo wa serikali moja katika katiba ijayo, vilevile tunataka watu ambao
watakuwa kwenye bunge la katiba wawe ni raia au watu wa kawaida, mashirika
mbalimbali(NGO’S) na wanasiasa wawe wachache wasiwe wengi”, alisema Manase.
Kadhalika alisema kituo cha sheria na haki za binadamu
wanatoa msaada wa kisheria na elimu kwa ujumla, ili watu waweze kuwa na uelewa
wa kupata haki zao za msingi.
Pamoja na mambo mengine mada kuu ambazo zimekuwa zikitolewa
katika mafunzo hayo ni sheria ya ajira na mahusiano kazini, haki za binadamu,
katiba, rushwa, haki kazi na wajibu wa madiwani, kanuni kuhusu maadili ya madiwani
na kukuza uelewa wa madiwani juu ya dhana kuu ya uwajibikaji na uwazi wa
shughuli za halmashauri.
No comments:
Post a Comment