Ludovick Utouh, Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali. (Picha kwa hisani ya mtandao) |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya wakazi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
wameishukuru serikali kwa kuchukua hatua ya kumleta Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa
hesabu za serikali hapa nchini(CAG) kufanya ukaguzi, katika halmashauri yao ya
wilaya hiyo.
Walisema hatua hiyo ni ya busara, na
inapaswa kuungwa mkono kutokana na halmashauri hiyo kuwepo malalamiko mengi miongoni
mwa jamii, juu ya utekelezaji mbovu wa miradi mbalimbali ya wananchi.
Baadhi ya miradi ya wananchi
wilayani Mbinga, imetekelezwa kwa kiwango kisichokubalika ikiwemo ujenzi wa
barabara za wananchi vijijini, miradi ya kilimo cha umwagiliaji, majosho ya
kuogeshea mifugo na hata nyumba za watumishi vijijini.
Wakazi hao kwa nyakati tofauti
walieleza kuwa hata kwa upande wa kitengo cha manunuzi wilayani humo wanamashaka
nacho, hivyo wameiomba serikali kuwa makini na kitengo hicho wakati
wanapokifanyia ukaguzi.
“Ukarabati wa majengo ya halmashauri hiyo kwenye idara
mbalimbali nao umekuwa ukifanywa kwa kutokidhi viwango, ambapo kuna tetesi
kwamba majengo mengine yamekuwa yakitengewa fedha na ukarabati wake umekuwa
haufanyiki, sasa tunahoji fedha husika zinapelekwa wapi?”, walisema.
Pamoja na mambo mengine Mwandishi wa
habari hizi alipozungumza kwa nyakati tofauti na baadhi ya wafanyakazi wa
halmashauri ya Mbinga, baadhi yao walisema ukaguzi huo umekuwa ni changamoto kubwa
kwao.
Wengine walisikika wakisema; “vichwa
vimekuwa vikituuma, matumbo joto juu ya ukaguzi huu, sijui hapa kama tutapona…..”.
Hata hivyo vyanzo mbalimbali vya
habari vimeeleza kwamba ukaguzi huu ni wa muda mfupi na hautachukua siku nyingi,
hivyo wanachosubiri ni kuona serikali inawatendea haki wananchi wa wilaya ya
Mbinga kwa kuibua ukweli uliopo na pale itakapobaini kuna matatizo wameitaka
serikali ichukue hatua mara moja, ili iwe fundisho katika jamii.
No comments:
Post a Comment