Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga. |
ENDAPO uongozi wa wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, utaendelea kupuuzia na kufumbia macho juu ya usimamiaji na
ujenzi bora wa miradi ya kilimo cha umwagiliaji, hakika maendeleo katika sekta
ya kilimo hicho cha umwagiliaji hapa wilayani yataendelea kudorola.
Siku zote jamii imekuwa ikitambua
kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote ile hapa duniani na ni
tegemeo kwa wataalamu husika waliopo katika sekta hiyo, kuendeleza miradi
mbalimbali ya kilimo hicho, ili wananchi wake hususani wakulima waweze
kuzalisha mazao yao shambani kwa ubora unaokubalika.
Mwandishi wa makala haya anaelezea juu
ya utata uliopo katika mradi wa umwagiliaji wa Sangamabuni uliopo kijiji cha
Mabuni kata ya Litumbandyosi, ambapo umekuwa ukizua malalalamiko kutoka kwa
wananchi kwamba ujenzi wake ulishindwa kuendelea kutokana na uongozi wa wilaya
hiyo, kushindwa kusimamia kikamilifu na kufuata taratibu husika za wataalamu wa
kanda ya umwagiliaji Mtwara.
Kana kwamba hilo halitoshi baadhi ya
miradi mingi ya kilimo cha umwagiliaji wilayani Mbinga, imejengwa kwa kiwango
cha chini kiasi ambacho imekuwa ikisababisha serikali kuendelea kuingia gharama
ya kuijenga upya, kutokana na miundombinu iliyojengwa awali kwa kiwango cha
chini kusombwa na maji.
Uchunguzi uliofanywa unabainisha
kwamba mradi huo wa Sangamabuni mkandarasi aliyepewa awali jukumu la kuujenga
ni GS Company Limited, alisaini mkataba wa ujenzi huo mnamo Agosti 29 mwaka
jana, na kupata kibali rasmi cha kuanza kazi ya ujenzi Novemba 22 mwaka jana
baada ya kushinda zabuni.
Lakini tokea mkandarasi huyo apewe
idhini ya kufanya kazi hiyo hadi leo hii mradi huo unashindwa kusonga mbele, na
badala yake katika eneo la ujenzi wa mradi, mkandarasi huyo amesogeza mawe tu
na hakuna kazi inayoendelea.
Wakulima walitegemea msimu wa mwaka
huu waanze kuzalisha mpunga, hivyo kutokana na mkandarasi huyo kutokamilisha
kazi yake kwa wakati wamebakia kwenye sintofahamu, na hawajui wafanye nini
licha ya malalamiko yao kuwepo mezani mwa viongozi wa wilaya ya Mbinga.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika
vimesema kuwa mradi huu tokea mkandarasi huyo apewe jukumu la kuujenga, kazi
hiyo ilitakiwa iwe imekamilika kwa muda wa miezi sita tokea aliposaini mkataba
husika, lakini hali bado ni tete na siku za ujenzi zimekwisha.
Takribani miezi kadhaa sasa imepita
utekelezaji wa mradi huu umekuwa ni utata mtupu, ambapo nimeshuhudia jinsi gani
ulivyo jambo ambalo limenifanya leo hii nifikie hitimisho kwa nafasi hii
kuelezea katika makala haya.
Kwa ujumla jambo la msingi
lililonigusa katika hili ni kwamba utekelezaji wa mradi huu umegubikwa na
madudu ambayo yanasababishwa na baadhi tu ya wataalamu wa halmashauri ya wilaya
ya Mbinga, ambao awali walipewa jukumu la kwenda kuupima na baadaye ufanyike
usanifu na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yaani ujenzi wa mifereji ya
kupeleka maji mashambani, kazi ambayo walishindwa kuifanya kutokana na kukosa
utaalamu wa ujenzi wa miradi ya umwagiliaji.
Vyanzo mbalimbali
vimeeleza kwamba timu ya watu watano kutoka halmshauri ya wilaya hiyo,
ilimwandikia barua aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, Shaibu Nnunduma ambaye sasa amehamishiwa wilaya ya Nyasa
mkoani humo, kumuomba gharama za uchunguzi na upimaji wa mradi huo wa
umwagiliaji Sangamabuni na mkurugenzi huyo aliwalipa fedha za kujikimu(posho)
na mafuta kwa ajili ya kuweka kwenye gari na kufikia jumla ya shilingi milioni
2,130,0000 ili waweze kwenda huko kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Barua hiyo waliyomwandikia ni ya
tarehe 11 Februari 2010 ambayo nakala yake tunayo, yenye kumbukumbu namba
MBWD/GF/II/Vol III/MM/28 ambayo ililenga kumuomba mkurugenzi atoe fedha hizo
huku ikiwa na majina ya wataalamu kutoka idara ya maji na kilimo wilayani humo
na kiasi cha fedha kwa kila mtumishi aliyelipwa ambao ni Amos Mtweve aliomba
kulipwa shilingi 270,000, Mohamed Machela 420,000, Christomus Nchimbi 420,000,
Alphonce Nakitundu 210,000 na Vincent Buriani 300,000 ambapo walipewa na mafuta
aina ya dizeli lita 300 yenye thamani ya shilingi 510,000 kwa ajili ya kuweka
kwenye gari ambalo liliwapeleka huko katika kijiji cha Mabuni ambako mradi huo
upo.
Kwa mujibu wa barua hiyo inasema
gharama hizo ni kwa ajili ya shughuli za upimaji tu na gharama za usanifu
zitakuja baada ya upimaji kufanyika, jambo ambalo linashangaza kwamba fedha
hizo wamelipwa na kazi hadi leo inaendelea kusuasua.
Pamoja na mambo mengine uongozi wa
kijiji hicho unasema wataalamu hao walishindwa kufanya kazi hiyo ya upimaji, na
kufikia hatua ya kumuomba Injinia wa kanda ya umwagiliaji Mtwara Pius Makaka na
wenzake, kwenda huko na kulazimika kufanya kazi hiyo ya upimaji ambayo iligharimu
shilingi milioni 16 ambazo halmashauri hiyo inalojukumu la kuwalipa kutokana
kazi waliyoifanya ya upimaji.
Baada ya kukamilisha michoro ya
upimaji huo injinia huyo alileta gharama ya mradi huo kwa Mkurugenzi huyo
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, shilingi milioni 574 ambazo
zinaweza kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
Gharama hizo zilipowasilishwa mezani
kwa mkurugenzi huyo wataalamu wawili kutoka idara ya maji na ujenzi katika
halmashauri hiyo, waliandika andiko la kuomba fedha katika ubalozi wa Japan
hapa nchini, ambapo walifanikiwa kupewa msaada wa shilingi milioni 275 ili
waweze kuanza kazi ya ujenzi huo.
Fedha hizo zilipotolewa ndipo tenda
ya ujenzi huo ilipotangazwa na kufikia hatua ya kampuni ya GS kushinda zabuni
husika, lakini utata uliopo inadaiwa kwamba kikwazo kinachosababisha mradi huo
usiweze kujengwa kwa wakati unatokana na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya
Mbinga, kutotaka kufuata taratibu za kitaalamu za michoro iliyochorwa na
injinia wa kanda ya umwagiliaji Mtwara na kulazimisha kutaka kufanya mambo
kienyeji kwa lengo la manufaa yao binafsi.
Wakati hilo likiendelea, injinia wa
kanda hiyo baada ya kuona siku zinazidi kwenda na mkandarasi husika tokea apewe
jukumu la ujenzi wa mradi huo hakuna kitu kinachoendelea, alimwandikia barua
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ya terehe 3 Oktoba 2012 yenye
kumbukumbu namba P/ZIU/M/02/09 kumshauri avunje mkataba wa mkandarasi huyo na
kutangaza zabuni upya ya ujenzi wa mradi wa Sangamabuni, jambo ambalo
lilichukua msuguano wa muda mrefu bila kutangazwa na kusababisha mivutano isiyo
ya lazima kati ya halmashauri hiyo na kanda ya umwagiliaji.
Katika barua hiyo nanukuu moja ya
kipengele kilichomtaka mkurugenzi huyo avunje mkataba kinasema, “Therefore by
using clause 62.2 (a) of the public procurement manual which says that
contractor stops work for 28 days when no stoppageof work is shown on the
current work program and the stoppage has not been authorized by the project
Manager, then this should be treated as a fundamental breach of the contract. I
advise you as a client to terminate the work and also to be advertise again”.
Kadhalika alipoulizwa kwa njia ya
simu mkurugenzi wa kampuni ya GS aliyejitambulisha kwa jina la Stephan Gamba
ambapo alikiri kutofanya kazi hiyo ya ujenzi kwa wakati, katika mradi huo wa
umwagiliaji Sangamabuni na kusema yeye amesogeza mawe tu katika eneo la mradi
na taratibu zingine za ujenzi zinafuata.
“Mwandishi ni kweli mradi huu sisi
ndiye tuliyeshinda zabuni, lakini ujenzi huu unakwamishwa na viongozi wenyewe
sisi hatujashindwa kuujenga”, alisema Gamba.
Pamoja na mambo mengine mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga alipoulizwa juu ya
utata huo amesema, yeye amechukua jukumu la kuvunja mkataba wa ujenzi wa mradi
huo wa umwagiliaji na kuutangaza upya kutokana na matatizo hayo yaliyopo, na
sasa aliyeshinda zabuni ya ujenzi huo ni kampuni ya Ovans Constraction Company
Limited.
Ngaga amesema ujenzi wa mradi wa
Sangamabuni wakati wowote kuanzia sasa mkandarasi huyo ataanza kazi ya ujenzi,
ili kuondoa malalamiko hayo yaliyokuwepo hapo awali.
Pamoja na mambo mengine leo naweza
kusema utekelezaji wa miradi mingi ya umwagiliaji kilimo cha mpunga wilayani
hapa, haijalenga matakwa yaliyowekwa na serikali licha ya kuwekeza fedha nyingi
katika miradi hiyo na ndio maana inajengwa kwa viwango visivyokubalika, kitendo
ambacho kimekuwa kikizua malalamiko mara kwa mara kutoka kwa wananchi.
Kwa ujumla ujenzi wa miradi ya
umwagiliaji wilayani Mbinga inakwama kutokana na viongozi husika kutowajibika
ipasavyo juu ya suala zima la kilimo kwanza.
Nimepita vijijini katika baadhi ya
miradi ambako inatekelezwa, malalamiko lukuki yamekuwa yakitolewa na wakulima
wakidai kuwa ujenzi mbovu wa mabanio na mifereji ya kupeleka maji mashambani
ndio kikwazo kikubwa kinachosababisha washindwe kutimiza adhma yao ya mapinduzi
ya kijani.
Nakumbuka serikali hapa nchini
iliitengea fedha halmashauri ya wilaya hiyo shilingi bilioni 1.5 mwaka 2005 za
ujenzi wa miundo mbinu ya miradi hiyo ya umwagiliaji, lakini matokeo yake ya
uzalishaji wa mazao ni hafifu kitendo ambacho kinazua maswali mengi miongoni
mwa jamii na bado serikali imekuwa ikitoa fedha kila mwaka kwa ajili ya
kuendeleza miradi hiyo.
Nashauri kuwa ni vyema serikali
kupitia wizara yake ya kilimo chakula na ushirika ikalifanyia kazi hili mapema
ili kuondoa malalamiko yaliyopo sasa hapa wilayani, kutoka kwa vikundi vya
wakulima ambavyo vimeundwa na vipo tayari kuzalisha zao la mpunga kwa njia ya umwagiliaji.
Ili tuweze kufikia malengo ya kauli
mbiu ya kilimo kwanza hapa nchini, sina budi kusema kuwa watendaji ambao
ni wazembe katika kusimamia suala zima la kilimo hicho ni vyema wawajibishwe,
ili iwe fundisho kwa watendaji wengine ambao ni wazembe katika kusimamia
maendeleo ya wananchi.
Siku zote watu wa Mbinga wengi wao
ni wachapa kazi hususani katika nyanja ya kilimo, na wanachohitaji ni usimamizi
tu kwa kuelekezwa mbinu bora za kilimo ili waweze kufikia malengo
waliyojiwekea.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
ninakumbuka mnamo mwezi Oktoba mwaka jana aliitisha mkutano hapa nchini,
uliowahusisha viongozi husika na kuwapa maagizo ya kilimo yaliyofikiwa katika
mkutano huo kuweka malengo ya kuinua kilimo katika mikoa sita ya Morogoro,
Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kigoma na Rukwa.
Ili tuweze kufikia malengo
yaliyofikiwa katika kikao hicho ni vyema sasa viongozi katika mikoa hiyo
hususani hapa wilayani Mbinga, tusimamie ipasavyo fedha zinazotolewa na
serikali ili tuweze kufikia malengo yaliyokusudiwa na miradi ya umwagiliaji
ijengwe kwa kufuata taratibu husika, sio kuishia kulumbana kila kukicha na
kusababisha maendeleo ya wananchi kushindwa kusonga mbele.
No comments:
Post a Comment