Tuesday, September 3, 2013

MAMA AJIFUNGULIA CHOONI BAADA YA KUFUKUZWA AKITOKEA KATIKA KITUO CHA AFYA

Rais Jakaya Kikwete.




















Na Steven Augustino,

Tunduru.

MKAZI wa kijiji cha Tunginya katika tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Zabibu Maulidi(16) amejifungua katika choo cha nyumba iliyopo karibu na barabarani kuelekea mjini Tunduru, wakati akisubiri usafiri wa kumpeleka hospitali ya wilaya hiyo.

Mashuhuda wa Tukio hilo akiwemo Mwenyekiti wa kata hiyo kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Ambali Kubodola alisema kuwa tukio hilo, lilitokea baada ya mgonjwa huyo kufukuzwa na Mkunga aliyekuwa zamu katika kituo cha afya kilichopo katika makao makuu ya tarafa ya Nakapanya Fafuma Amamu Chakilo akidai kuwa mgonjwa huyo alipewa maelekezo ya kwenda kujifungulia katika hospitali yenye Madaktari.

Mume wa Binti huyo Salum Said alisema kuwa  baada ya tukio hilo la kutimuliwa Zabibu ambaye alikuwa ameongozana nae walitoka katika eneo hilo la Kituo cha afya, wakiwa hawaelewi cha kufanya hali ambayo iliwafanya wakae katika kituo cha mabasi lakini baada ya muda mkewe huyo alishikwa na uchungu, lakini kutokana na kutoelewa kinachoendelea alienda katika nyumba hiyo na kuomba hifadhi ya kujisaidia.



Alisema akiwa ndani ya choo hicho ghafla yeye na mashuhuda wengine walisikia kelele na kishindo kikubwa baada ya kwenda walimkuta akiwa ameanguka chini huku akiwa ameiishiwa nguvu, na kuanguka pembeni na kujifungua papo hapo mtoto wa kiume, hali ambayo ilimfanya apoteze fahamu kwa muda ambapo baada ya tukio hilo walimjulisha Diwani wa kata ya Nakapanya Mfaume Wadali ambaye alifika katika eneo la tukio na kuamuru apelekwe katika kituo hicho, kwa ajili ya matibabu.

Akizungumzia sakata hilo diwani huyo alisema kuwa baada ya kufika katika Kituo hicho na kumuhoji Mkunga huyo, alimweleza kuwa chanzo cha kutopatiwa huduma mgonjwa huyo, kilitokana na maelekezo yaliyokuwa yametolewa katika kadi yake ya kliniki ambayo iliwekwa alama nyekundu kuwa anatakiwa kujifungulia  hospitalini na sio katika kituo cha afya.

Alisema hata hivyo alimruhusu kwenda kusubiri usafiri katika kituo cha mabasi baada ya kumpima na kujiridhisha kuwa uchungu wake ulikuwa bado upo mbali sana, na kwamba kama angepata usafiri mapema angeweza kufika katika hospitali hiyo iliyopo umbali wa kilometa 60 kutoka katika kituo hicho cha afya.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya Simu kaimu Mganga mkuu wa hospitli ya wilaya hiyo Dkt. Bernad Mwamanda mbali na kudhibitisha kuwepo kwa tukio hilo, alitoa wito kwa wajawazito kufuatilia maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na maafisa tabibu ili kuokoa maisha yao na watoto wanaojifungua.

Alisema endapo wataendelea kuwa wakaidi wa kufika mapema hospitalini kujitazamia kabla ya kupata uchungu, watakuwa wanajiweka katika hatari ya kupoteza maisha yao na watoto wao na kwamba juu ya tukio hilo wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha hali ilivyotokea na kwamba hawatasita kuchukua hatua endapo watabaini kulikuwa na uzembe umefanyika.
 

No comments: