Kanisa la Mtakatifu Killian lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma. |
Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Senyi Ngaga, naye hakuwa mbali katika kushiriki maadhimisho ya misa takatifu ya kuwapaka watoto mafuta ya Kipaimara. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WAUMINI wa dhehebu la Kikristo, wameshauriwa kutojiingiza
katika matukio yenye kuhatarisha na kuvuruga amani ya nchi yetu, na badala yake
waungane kwa pamoja kupinga matukio maovu yanayoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali
hapa nchini.
Wito huo ulitolewa na Balozi wa Papa hapa nchini, Askofu mkuu
Francisco Montecillo Padilla alipokuwa akizungumza na Waumini wa Kanisa la
Mtakatifu Killian Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, katika maadhimisho ya sherehe
za misa takatifu ya kuwapaka mafuta ya daraja la kipaimara, watoto waliokuwa wakipatiwa daraja hilo.
Balozi huyo alisema itakuwa si busara kwa waumini wa dhehebu
hilo kujihusisha na matendo yasiyompendeza Mungu, hivyo ni vyema wajiepushe ili
taifa liendelee kuwa na amani.
“Ndugu zangu matukio ya ajabu yamekuwa yakiendelea kutokea,
mapadri wamekuwa wakifanyiwa vibaya kule Zanzibar, makanisa yetu yanachomwa
moto, kwa kweli matukio kama haya hayavumiliki na haya mpendezi Mungu”, alisema Padilla.
Aidha wakati wa maadhimisho ya misa hiyo ulinzi mkali ulikuwa
umetanda kuzunguka kanisa hilo ndani na nje, ambao ulijumuisha maofisa usalama
wa taifa na askari polisi huku waumini wa kiislamu ambao walionekana kutaka
kuingia katika eneo la kanisa hilo, walizuiwa kuingia.
Vyanzo mbalimbali vya habari ambavyo vilizungumza na
mwandishi wa habari hizi vilisema kuwa kuzuiwa huko, kulitokana na kuhusishwa
kwa matukio mabaya yanayoendelea kufanyika hapa nchini hususani kwa lile la
mlipuko wa bomu huko Arusha, ambalo lilitokea hivi karibuni.
Kadhalika wengine walikuwa wakisema wachungaji na mapadre
kule Zanzibar nao wamekuwa wakiumizwa na kupata mateso na makundi ya waislamu
ambayo hayana nia njema na wakristo, na kwamba wamechoshwa na vitendo hivyo na
kuitaka serikali ichukue hatua madhubuti za kisheria kwa wale wanaohusika.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa jimbo la Mbinga John Ndimbo
naye alisema hivi sasa katika kipindi hiki kigumu, amewataka wakristo nchini kuwa na umoja na kutolipiza kisasi kwa matukio
mabaya wanayofanyiwa kama vile kushambuliwa kwa mapadre na kuchomewa moto
makanisa, badala yake wawe watulivu na kuendelea kumwomba Mungu na yeye ndiye
mwenye kujua nani anastahili kupewa adhabu kwa yule mwenye makosa.
No comments:
Post a Comment