Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Juma Simai, akifungua jengo(Ghala) la kampuni ya BAM ambalo hutumika kuhifadhia pembejeo za kilimo. |
Uongozi wa kampuni ya BAM ukiwa katika picha ya pamoja na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Juma Simai.(aliyeshika Mwenge) |
Hizi ni moja kati ya pembejeo za kilimo ambazo husambazwa na kampuni ya BAM kwa wakulima mkoani Ruvuma. |
Mkurugenzi mkuu wa BAM, Bernad Malila. (Picha zote na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KIONGOZI wa mbio Mwenge wa Uhuru Juma Simai ameipongeza
kampuni ya BAM (LTD) inayojishughulisha na usambazaji wa pembejeo za kilimo katika
maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma, kutokana na kuwa na mipango thabiti
inayolenga kupanua shughuli za kilimo na kuongeza uzalishaji wa chakula hapa
nchini hatua ambayo inaweza kuinua uchumi wa wakulima na nchi kwa jumla.
Simai alitoa pongezi hizo hivi karibuni mjini Mbinga, wakati
akifungua jengo la ghala la kuhifadhi pembejeo za kilimo lenye uwezo wa
kuhifadhi zaidi ya tani 600 za mbolea aina mbalimbali na kuiagiza serikali ya
wilaya ya Mbinga, kuunga mkono juhudi kubwa iliyoonyeshwa na kampuni hiyo kwani
inalenga kuwakomboa na kuwasaidia wakulima.
Alisema iwapo viongozi watashirikiana na BAM katika mkakati wa
kitaifa wa kukifanya kilimo kiwe ni kati ya maeneo makubwa ya kiuchumi, kuna
uwezekano mkubwa wa wilaya hiyo kupiga hatua za haraka za maendeleo kufuatia
kuwepo kwa eneo kubwa la ardhi inayofaa kwa ajili ya shughuli za kilimo
ikilinganishwa na maeneo mengine hapa nchini.
Alieleza kuwa kitendo
cha kampuni hiyo kupunguza bei za pembejeo ni faraja kubwa siyo kwa wakulima
pekee, bali hata kwa serikali kwani nayo imepania kukifanya kilimo kiwe ni eneo
lingine la kibiashara zaidi kwa kuajiri maafisa ugani wengi na kupunguza ruzuku
na kodi katika vifaa vya kilimo, hivyo ni vyema kila mmoja wakiwemo viongozi
kushiriki na kuiunga mkono kampuni hiyo ambayo imeleta unafuu mkubwa kwa
wakulima wa wilaya ya Mbinga, mkoa na taifa kwa ujumla.
“Viongozi wa Mbinga, wapeni ushirikiano hawa watu
wanaokuja kuleta maendeleo hapa wilayani kwenu, narudia kulisema
hili kwa sababu viongozi katika maeneo mengi tumekuwa watu wa kujisahau sana, hakuna
maendeleo ya kweli yanayokuja bila ya kushirikiana na wadau”, alisema Simai.
Awali akitoa taarifa ya kampuni hiyo Meneja mkuu wa kampuni ya BAM
Suzo Komba alieleza kuwa lengo kubwa la mradi huo ni kuleta huduma za
usambazaji wa pembejeo kwa wakulima wakubwa na wadogo katika maeneo ya karibu
zaidi mkoani Ruvuma, ili kuwarahisishia upatikanaji wa pembejeo na
mahitaji mengine ya wakulima badala ya kutembea umbali mrefu kufuata pembejeo
za kilimo.
Komba alitaja walengwa wakuu katika mpango huo ni wakulima wa
mazao ya mahindi, kahawa, mpunga na mazao mengine ya chakula na biashara ambayo
kwa kiasi kikubwa yanazalishwa katika wilaya ya Mbinga na kuwa na kituo
kikubwa cha usambazaji na kitakacholinda ubora wa mbolea zitakazouzwa
kupitia kampuni hiyo.
Alisema hadi sasa kampuni hiyo imeweza kujenga ghala kubwa la
kuhifadhia mbolea ambalo limegharimu zaidi ya shilingi milioni 235.7 fedha
ambazo zimetokana na mfuko wa kampuni hiyo kutokana na faida kidogo wanazopata
baada ya kuuza pembejeo za kilimo, wanazozisambaza na kwamba aliishukuru
serikali chini ya wizara ya kilimo na chakula kwa ushirikiano mkubwa
wanaouonyesha kwa wasambazaji wa pembejeo za kilimo.