Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALI ya kisiasa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma,
imeendelea kuwa katika hali mbaya yaani sintofahamu, kufuatia Makao makuu ya
Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa kusitisha zoezi la uchaguzi wa nafasi ya
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, kutokana na vurugu zilizojitokeza.
Usitishaji huo umefanyika leo majira ya saa 10:00
baada ya Katibu wa CCM wa mkoa huo Verena Shumbusho kutoa taarifa mbele ya
Madiwani wa wilaya hiyo kwamba, uchaguzi huo hauwezi kufanyika mpaka taarifa
rasmi itakapotolewa kutoka ofisi ya makao makuu ya chama hicho.
Sababu za msingi za kutofanyika kwa uchaguzi huo
zimebainishwa katika kikao hicho kilichoketi kati ya Katibu huyo, Madiwani na Uongozi
wa Chama hicho wilaya ya Mbinga, ambapo Shumbusho alieleza bayana mbele ya Wajumbe
(Madiwani) kwamba wawe na subira mpaka taarifa hiyo itakapotolewa juu ya
kufanyika kwa uchaguzi huo, kwamba utafanyika lini.
Wajumbe ambao ni madiwani waliokuwepo kwenye ukumbi
wa CCM ambako mkutano huo wa dharula ulikuwa ukifanyika, ndani ya kikao hicho
walimweleza Katibu wao wa mkoa wa Ruvuma wa chama cha mapinduzi kwamba, endapo
kama watataka kuwepo na amani ni vyema majina matatu ya wagombea wa nafasi ya
Mwenyekiti yarejeshwe na sio kuletewa majina mawili kama ilivyokuwa awali.
Wengine walionekana kujawa jazba huku wakisema
hawapendi tabia za viongozi wa wilaya na mkoa kwa ujumla, kuwapangia safu za
uongozi hivyo wanachohitaji itumike demokrasia huru na yenye haki.
Hatua hiyo imefikia kufuatia Madiwani hao kujenga
msimamo wa kutokubali kufanya uchaguzi huo, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa
uongozi wa CCM mkoa wa Ruvuma, kutotenda haki katika uteuzi wa majina ya
wagombea wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Hali si shwari ambapo baadhi ya madiwani walionekana
wakija juu na kuutaka uongozi husika kutenda haki, na kwamba ifikapo kesho Juni
22 mwaka huu halmashauri ya wilaya ya Mbinga inatarajia kuvunja baraza lake la
madiwani ili kujenga uongozi wa pande mbili za wilaya ya Mbinga na Nyasa.
Wilaya ya Nyasa imekwisha fanya uchaguzi lakini kwa
upande wa wilaya ya Mbinga, imeshindwa kufanya uchaguzi kutokana na vuguvugu
hilo ambalo bado linaendelea kufukuta wilayani humo.
Hivyo kwa siku ya kesho ambayo Madiwani wanataraji
kuvunja baraza la halmashauri kwa upande wa wilaya ya Mbinga ambako hakuna
uchaguzi uliofanyika, utaratibu unasema kwamba wilaya hiyo katika kikao cha
kuvunjwa kwa baraza hilo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya,Chiristantus Mbunda ndiye
atakayeweza kusimamia mustakabali mzima wa zoezi hilo kwa upande wa Mbinga.
Taarifa zilizotufikia hivi punde zinaeleza kwamba
wilaya ya Nyasa aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Oddo
Mwisho ndiye ambaye amepata ushindi wa kuongoza wilaya ya Nyasa huku makamu
wake akiwa bwana Vurma Whero. (Matokeo zaidi tutawajulisha juu ya uchaguzi huo
wa wilaya ya Nyasa ulivyofanyika.)
Awali Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani
Mbinga walionekana wakisota kwa muda mrefu, katika eneo karibu na viwanja vya
ofisi ya chama hicho wakisubiri hatma ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti, wa
kuongoza halmashauri ya wilaya hiyo.
Madiwani hao ambao walionekana wakiwa na jazba huku
wengine wakisema “hapa leo hakitaeleweka endapo kama hatutatendewa haki kwa
kile kinachotakiwa”.
Mwandishi wa habari hizi alifanya mahojiano na
madiwani hao kwa nyakati tofauti ambapo walisema wanachosubiri ni hekima ya
chama na kama hakutakuwa na busara ambayo itatumika wao hawatelewa kitu na
msimamo wao utaendelea kubaki pale pale.
Awali kufuatia vurugu hizo, katika hali isiyokuwa ya kawaida usiku wa kuamkia leo ofisi ya
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imenusurika
kuteketea kwa moto kufuatia watu wasiojulikana, kuichoma moto kwa kutumia
mafuta aina ya petroli.
Ofisi
hiyo imechomwa madirisha na mlango mmoja huku ndani yake mapazia yaliyowekwa
madirishani, yakiwa yameteketea kwa moto.
Katibu
wa CCM wilaya ya Mbinga Anastasia Amasi alisema kuwa yeye akiwa nyumbani kwake
alipata taarifa za kuchomwa moto kwa ofisi hiyo majira ya saa 2:07 asubuhi ya
leo, ambapo alipofika katika eneo la tukio aliona uharibifu huo ukiwa umekwisha
fanyika.
Taarifa
zilizotufikia zinaarifu kwamba huenda Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
akawasili kesho hapa Mbinga, kwa ajili ya kuweka sawa hali hii ya upepo wa kisiasa
ili isiweze kuendelea kuvurugika. (Ndugu Wasomaji wa mtandao huu, tutaendelea kuwajuza nini
kinachoendelea juu ya tukio hili, endelea kufuatilia mkasa huu kupitia mtandao
huu)
No comments:
Post a Comment