Na Kassian
Nyandindi,
WAHENGA siku zote husema elimu ndio ufunguo wa maisha, na
hakuna sehemu ambayo inaweza ikawa na maendeleo pasipo kuwa na elimu.
Katika hili hatuna budi viongozi tukawa na mipangilio mizuri
ya kukuza sekta ya elimu katika maeneo yetu tunayofanyia kazi, kwa kujenga
ushirikiano na kubuni njia mbadala za kukuza taaluma mashuleni.
Ni aibu kuona viongozi siku zote tumekuwa tukilumbana na
kujenga migogoro ambayo inarudisha nyuma sekta hiyo muhimu, ambayo ndio msingi
wa maendeleo katika jamii.
Katika makala haya napenda kuelezea mgogoro wa idara ya elimu
shule za msingi, ambao umekuwa ukiendelea wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, na
kusababisha baadhi ya vigogo kulumbana pasipo kuwa na sababu zozote za msingi.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa vigogo
wachache wilayani humo, wameanzisha mgogoro huu kwa maslahi yao binafsi ambayo
hayana tija katika jamii.
Hivyo basi, kutokana na kushamiri kwa upuuzi huo
kunasababisha kuwavunja moyo baadhi ya watendaji wa idara ya elimu msingi
wilayani hapa, ambao wanaonekana kujituma katika kufanya kazi zao kwa umakini.
Upuuzi huo ni ule wa kuandikiana barua za kuchafuana ambazo imefikia
hatua zinaleta mtafaruku ambao naweza kusema, tusipokuwa makini taifa la
Wanambinga tutalifikisha pabaya.
Nashauri ni vyema sasa tukaacha mambo haya tubakie katika
mstari wa kuendeleza sekta hii muhimu, na sio kuishia wakati wote kulumbana na
kujengeana bifu ambazo hazina mantiki yoyote ile.
Nimebaini pia ugonvi huu wakuandikiana mabarua ya kuchafuana
yanatokana na kigogo mmoja(Jina tunalo) hapa wilayani, kuendekeza tabia ya
kukataa watumishi wanaohamishiwa hapa na kutaka apange safu yake anayoitaka
yeye, ili aweze kufuja vizuri fedha za idara hiyo ya elimu.
Ndugu zangu hili halingii akilini, haya mambo yamepitwa na
wakati kinachotakiwa sasa ni kukaa pamoja na kufanya kazi kama timu, vinginevyo
tusipozingatia hili mwisho wa siku elimu hapa wilayani itaendelea kudorola na
kufikia mahali pabaya.
Kama tutafikia hapo taifa hili la kizazi cha sasa na kijacho,
halitatuelewa badala yake litatuadhibu kwa kutupiga viboko kutokana na dhambi
hii tunayoifanya sasa.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, kilio cha Wanambinga
wanakutaka udhibiti tatizo hili lisiweze kuendelea, maana wewe ndio mhimili
mkuu wa maendeleo hapa wilayani.
Wanambinga wanasema viongozi wanaofanya vurugu hizo za kutaka
kurudisha nyuma maendeleo ya elimu unawafahamu na wapo katika mafaili yako
mezani, hivyo wanakuomba usiwafumbie macho wachukulie hatua ikiwezekana hata
kuwahamisha waondoke hapa Mbinga.
Pia wanasema wamechoshwa na tabia hii, na endapo wataona
inaendelea wapo tayari kuandamana hadi ofisini kwako, wakipinga vitendo hivyo
ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu.
Nionavyo, leo wilaya ya Mbinga maendeleo ya elimu ya msingi yanaanza
kuonekana kung’ara, sasa najihoji mwenyewe ni mdudu gani ambaye anataka
kuturudisha nyuma tulikotoka, ambako kulikuwa kubaya kiasi ambacho ilikuwa ni
aibu tupu?
Leo walimu huko vijijini wilayani Mbinga, nimeshuhudia jinsi
gani wanavyojituma wakati huu walikizo kufundisha watoto wanaotarajia kumaliza
darasa la saba, wanapaswa kupongezwa katika hili.
Vituo vya kufundishia vimewekwa kwa kila kata, watoto
wanasoma vizuri bila matatizo yoyote yale, wazazi wanashiriki vyema katika
kutoa michango yao ili ufanisi mzuri uweze kuwepo.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, natambua kilio chetu umekisikia na
utakifanyia kazi hivyo tunachotarajia sasa ni kuona matunda mema na mgogoro huu
hatutaki kuuona ukiendelea, yule ambaye utambaini anaendekeza mambo haya ni vyema
awajibishwe kwa namna moja au nyingine, ili iwe fundisho kwa wengine wenye
tabia kama hiyo.
Mungu ibariki Mbinga, Ruvuma na Tanzania kwa ujumla,
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu namba
0762578960.
No comments:
Post a Comment