Upande wa kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga akizungumza na wadau mbalimbali wilayani Mbinga hivi karibuni. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amemshukia Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
tawi la Mbinga Samwel Mhaiki, akidai kwamba ni kikwazo cha maendeleo ya elimu
wilayani humo, kutokana na katibu huyo kupenda kuendesha migogoro na kuchonganisha
walimu mashuleni.
Ngaga alisema hayo alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, juu ya maendeleo ya sekta ya elimu
ya wilaya hiyo.
Alisema kuwa katibu huyo
amekuwa kinara namba moja wa kupita mashuleni na kushinikiza walimu waache
kufundisha (Wagome) hadi watakapolipwa madai yao, jambo ambalo alilieleza kuwa
limekuwa likileta mgogoro usio na tija katika jamii.
Alieleza kwamba yeye na
kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mbinga, walimwita Mhaiki na
kuketi naye pamoja wakimtaka aache kuendeleza mgogoro huo na alikiri kutofanya
hivyo lakini wanashangaa kumuona akiendelea.
“Mimi na kamati yangu ya
ulinzi na usalama tulimwita katibu huyu wa CWT lakini amekuwa akitusumbua sana,
anaandika barua na kuzisambaza mashuleni akishinikiza walimu wagome waache
kufundisha, tulimwambia serikali inashughulikia madai ya hawa walimu na
watalipwa,
“Akatuomba radhi na kusema
hatarudia tena, malumbano haya anayoyaendeleza sasa ningelikuwa na uwezo mimi
nikiwa Mkuu wa wilaya hii ningemhamisha, kwa sababu ni kikwazo kwa maendeleo ya
elimu hapa wilayani, leo walimu wakigoma watoto wetu watafundishwa na nani”,
alisema Ngaga.
Mkuu huyo wa wilaya ya
Mbinga awali alisema wilaya yake hivi sasa imejipanga katika kukuza kiwango cha
elimu kwa shule za msingi na sekondari, ambapo hivi sasa kwa kushirikiana na
ofisa elimu wa wilaya hiyo Mathias Mkali wameanzisha utaratibu wa watoto wanaotarajia
kumaliza darasa la saba hivi karibuni, wameweka vituo vya kujisomea (Makambi)
kwa kila kata mashuleni wilayani humo wakati huu wa likizo ili waweze kujiandaa
na mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi.
Alisema wazazi wameitikia
wito kwa kiasi kikubwa juu ya suala hilo na kukubaliana kutoa michango ya chakula,
katika vituo hivyo ambavyo watoto wao wanasoma.
Pamoja na mambo mengine
alisisitiza kuwa mtu yeyote atakayeonekana anakwamisha mikakati waliyojiwekea
ya kukuza kiwango cha elimu wilayani Mbinga, yupo tayari kumwajibisha ili iwe
fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment