Christantus Mbunda, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
UCHAGUZI wa nafasi ya Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambao uliahirishwa siku kadhaa
zilizopita, sasa unatarajiwa kufanyika rasmi kesho Juni 29 Mwaka huu, katika
ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo mjini hapa.
Kamati kuu ya chama hicho makao
makuu ya taifa ilichukua jukumu la kuahirisha uchaguzi huo, kutokana na vuguvugu
la kisiasa lililoshamiri mjini hapa ambalo linadaiwa kusababisha hata uchomaji
moto wa ofisi ya Katibu wa CCM na kunusurika kuungua kabisa.
Vurugu hizo zinadaiwa kupinga ubabe
uliokuwa umefanywa na kamati ya siasa ya mkoa huo, ambayo inashutumiwa kukata jina la mgombea
mmojawapo kimakosa kwa maslahi yao binafsi.
Ukataji wa jina hilo ambalo ni la Diwani
Allanus Ngahi wa kata ya Kipapa, ulisababisha Wajumbe kugoma kufanya uchaguzi
hadi watakapopata ukweli juu ya kwa nini jina hilo lilikatwa kimakosa au la.
Lakini baada ya kuona hali inazidi
kuwa mbaya ndio Kamati kuu ya chama cha mapinduzi taifa ilichukua jukumu la
kuahirisha uchaguzi huo, mpaka itakapoyafanyia kazi madai hayo ya madiwani
waliogoma kufanya uchaguzi huo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida
ofisi ya Katibu huyo ilinusurika kuteketea kwa moto kufuatia watu
wasiojulikana, kuichoma moto kwa kutumia mafuta aina ya petroli.
Ofisi hiyo ilichomwa
madirisha na mlango mmoja huku ndani yake mapazia yaliyowekwa madirishani,
yakiwa yameteketea kwa moto.
Akizungumza na Mwandishi
wa habari hizi Katibu wa CCM wa wilaya ya Mbinga Anastasia Amasi alisema, uchaguzi
huo unafanyika kesho kutokana na Kamati kuu ya chama hicho kurejesha majina ya
wagombea sita ambao waliomba kuwania nafasi hiyo.
Alisema nafasi ya
Mwenyekiti inagombewa na majina matatu ambayo ni Allanus Ngahi kutoka kata ya
Mpapa, Nathaniel Challe kata ya Matiri na Allan Mahay kata ya Maguu.
Kadhalika kwa nafasi ya
Makamu Mwenyekiti ni Agness Mahangula Diwani viti maalum kata ya Mbuji, Prisca
Haulle viti maalum kata ya Namswea na Winfrid Kapinga kata ya Ngima.
No comments:
Post a Comment