Na Steven Augustino, 
Tunduru.

MKUU wa  wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Chande Nalicho, amewataka vijana na makundi mengine yanayonufaika kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali wilayani humokuzingatia mafunzo hayo  ili yaweze kuwanufaisha na kuwa chachu ya kujiletea maendeleo miongoni mwao.
 
Nalicho alitoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya siku 10 yaliyotolewa kwa washiriki 55 juu ya uhifadhi wa udongo, maji na mazingira yaliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii kilichopo kijiji cha  Nandembo wilayani humo.

Pamoja na mambo mengine mkuu huyo wa wilaya, aliahidi kufanya ziara ya ufuatiliaji wa utekekelezaji wa mafunzo hayo kwa vitendo ifikapo Mei 31 mwakani na pia aliwasisitiza washiriki hao kueneza elimu waliyoipata kwa wengine na kuwawezesha kushiriki pamoja katika mapambano hayo ya uhifadhi wa mazingira.


Awali akisoma taarifa ya mafunzo hayo Katibu wa kikundi hicho Gerald Mayaya alisema kuwa katika kipindi hicho walifundishwa mbinu mbalimabli za utunzaji wa mazingira, utunzaji wa udongo na maji mashambani, maji na usafi wa mazingira, uvunaji wa maji na uhifadhi wa mazingira, sera, sheria mama ya mazingira na sheria ndogo ya mazingira pamoja na teknolojia ya umeme tungamo taka ( Bayoges ) inayotumia vinyesi vya mifugo na binadamu. 

Mratibu wa mafunzo hayo Kenedi Haule alimweleza Nalicho kuwa mafunzo hayo ambayo yamedhaminiwa na benki ya maendeleo ya Afirica ( ADB ) kupitia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini  ya mradi wa usimamizi wa ofisi ya Bonde la Maji pwani ya Kusini ya mto Ruvuma  yenye makao makuu mkoani Mtwara.

Hivyo utaweza kunufaisha wananchi wa wilaya hiyo katika vijiji vitatu ambavyo ni Lelolelo, Majimaji na Nandembo ambavyo tayari wananchi wake wamekwishapatiwa mafunzo hayo.