Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIBU wa Chama cha walimu Tanzania
(CWT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma Samwel Mhaiki amenusurika kipigo kutoka
kwa wanachama wa chama hicho, katika kikao na waratibu elimu kata wakimtuhumu
kukitumia chama hicho kwa maslahi yake binafsi na kutotekeleza majukumu yake
ipasavyo.
Kadhalika wanachama hao walidai
kwamba amekuwa akiwachonganisha walimu pamoja na viongozi wa serikali wilayani
humo.
Wakizungumza huku wakiwa
na jazba na wengine kutoa lugha chafu kwa Katibu huyo katika kikao
kilichowakutanisha waratibu elimu kutoka kata zote za mbinga na nyasa, pia
wamemtaka kuachia nafasi yake wakidai kuwa ameshindwa kuwasaidia katika kazi za
utumishi wa umma.
Walisema badala yake amekuwa mmoja
wa watu wanaotumika vibaya na baadhi ya viongozi wanaotaka kumuondoa afisa
elimu ya msingi Mathias Mkali, ambaye anaonekana ni mwiba kwa baadhi ya
vigogo wa halmashauri ya Mbinga wanaotajwa kuhusika na matumizi mabaya ya fedha
za malipo mbalimbali ya walimu.
Aidha Katibu huyo anadaiwa kuandika
barua na kuzisambaza katika shule zote za Mbinga kuzuia mpango wa masomo ya
ziada(makambi) hadi serikali itakapowalipa madai yote wanayodai, pamoja na
posho za kufundisha masomo hayo wakati wa likizo bila ya kupata ushauri kutoka
kwa wanachama ambao ni walimu na hata kwa viongozi wenzake akiwemo mwenyekiti
wake wa CWT.
Mwalimu Edmund Hyera wa shule ya
msingi Juhudi kutoka kata ya Kigonsera alieleza kuwa, barua aliyoiandika inaonesha
bado anaendelea na uchochezi kati ya serikali na walimu jambo ambalo
lilishakwisha tangu mwaka jana kufuatia ahadi mbalimbali za viongozi akiwemo
Rais Jakaya Kikwete, aliyehaidi kuyafanyia kazi madai yote ya walimu.
Alisema Mhaiki amekuwa mstari
wa mbele kutetea malsahi yake binafsi na sio ya walimu, ndiyo maana amefikia
hatua hata ya kuwachonganisha na mwajiri wao jambo linaloweza kuirudisha nyuma
wilaya yao kitaaluma, kwani muda mwingi viongozi wa serikali akiwemo afisa
elimu ya msingi hutumia muda mwingi wa maendeleo kutafuta suluhu ya matatizo
yaliyokuwepo jambo linaloashiria kutokuwepo kwa ushirikiano wa kutosha.
Aliongeza kuwa barua ya kuzuia
makambi kwa vijana wanaojiandaa kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya
msingi miezi miwili ijayo, inaonesha jinsi gani Katibu huyo alivyokuwa
adui namba moja wa elimu ya msingi Mbinga.
“Huyu katibu sio mtu mwema kwetu
sisi walimu amekuwa msaliti mkubwa kwetu ona yeye badala ya kushughulikia
matatizo yetu anajiingiza katika mambo yasiyomuhusu, ambayo ni sumu mbaya kwa maendeleo
ya elimu hapa mbinga”, alisema Hyera.
Pia alisema hadi sasa walimu
wamechoshwa na migogoro ya mara kwa mara inayosababisha kuwavunja moyo wa
kazi ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa.
Wanachama hao wamefika mbali zaidi
na kutishia kutaka kujitoa uanachama katika chama hicho na kuanza
kufikiria kujiunga na chama cha walimu cha Msumbiji ambako ni jirani zaidi
ikilinganishwa na Mbinga huku wengine zaidi ya walimu 40 kutoka kata ya Liparamba
wamekwisha andika barua za kujitoa uanachama wa CWT wilayani Mbinga.
Hata hivyo Mratibu elimu kata ya
Lipingo Alfred Chikoola amewataka viongozi wa chama hicho wilayani humo, kuacha
unafiki na kujiingiza katika migogoro ambayo haina manufaa katika jamii badala yake wawe wanaunga mkono maendeleo ya
elimu wilayani hapa kwa kujenga ushirikiano endelevu.
No comments:
Post a Comment