Na
Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANACHAMA
wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, leo wamekamilisha adhima
yao ya kuwachagua viongozi watakao waongoza katika nafasi ya Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya hiyo, uchaguzi ambao awali kulikuwa na mvutano na utata mkubwa
ambao ulisababisha hata kuzua vurugu za hapa na pale.
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida amani na utulivu vilitawala, huku askari polisi nao
wakionekana kuwa imara katika viwanja hivyo vya ukumbi wa CCM mjini hapa,
ambako uchaguzi ulikuwa ukifanyika.
Ni
tukio la pekee ambalo wapenzi na wafuasi wa chama hicho leo hii, walikuwa wakilisubiri
kwa hamu, juu ya nani ambaye anaweza kushika nafasi hiyo muhimu hapa wilayani.
Mara
baada ya uchaguzi huo kufanyika Katibu wa Chama hicho Anastasia Amasi,
alitangaza matokeo mnamo majira ya 8:35 ambapo alisema nafasi ya Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya ya Mbinga imechukuliwa na ndugu Allanus Ngahi ambaye
alipata ushindi wa kura 29.
Aliyefuatia
alipata kura 13 ambaye alikuwa ni Allan Mahay na wa mwisho alikuwa Nathaniel
Challe aliyepata kura 3.
Kwa
upande wa nafasi ya Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo mshindi alikuwa ndugu
Winfrid Kapinga, alipata kura 25 huku akifuatiwa na Prisca Haulle aliyepata
kura 19.
Pamoja
na mambo mengine hali ya uchaguzi ilikwenda vizuri huku Mbunge wa jimbo la
Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo, mara baada ya Katibu huyo kutangaza matokeo hayo,
aliwataka wajumbe waendeleze mshikamano katika kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ya wananchi wa Mbinga.
Shamra
shamra za hapa na pale zilitawala leo katika viwanja vya Chama cha Mapinduzi wilayani humo, huku
makada mbalimbali wa chama hicho wakionekana kufurahi na kuimba nyimbo
mbalimbali za chama na za kumtukuza Mungu.
Kwa
ujumla majina matatu yaliyogombewa katika nafasi hizo, Diwani Allanus Ngahi anatoka
kata ya Mpapa, Nathaniel Challe kata ya Matiri na Allan Mahay kata ya Maguu.
Kwa
nafasi ya Makamu Mwenyekiti Agness Mahangula Diwani viti maalum kata ya Mbuji,
Prisca Haulle viti maalum kata ya Namswea na Winfrid Kapinga kata ya Ngima.
No comments:
Post a Comment