Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imekutana jana tarehe 10/06/2013
chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Dr. Jakaya Mrisho
Kikwete. Kikao hicho kilikuwa cha siku moja na maalum kwa ajili ya
kupokea rasimu ya katiba mpya.
Kamati Kuu inaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini kwa kazi nzuri na kukamilisha kazi kwa wakati.
Kamati Kuu imepokea rasimu hiyo na kuelekeza kuwa;
Kwa kuwa rasimu hii ni ya kwanza ambayo inapelekwa kujadiliwa tena kwa
wananchi kupitia mabaraza mbalimbali ya katiba baada ya kuisha kwa hatua
ya kutoa maoni.
Kamati
Kuu imekiagiza Chama kijipange kuijadili rasimu hiyo ndani ya Chama
kama baraza la kitaasisi la katiba na kuwataka wanachama na wapenzi wa
CCM wajitokeze kwa wingi na kushiriki kwenye mabaraza haya.
Ushiriki huu wa CCM baada ya kupokea rasimu umekusudia kushirikisha wanachama wetu kwenye ngazi ya tawi, wilaya, mkoa na Taifa.
Lakini
pia Jumuiya za CCM zimekusudia kushiriki kama mabaraza ya Katiba na
hivyo kuongeza ushiriki wa wanachama na wapenzi wa CCM katika mchakato
huu.
CCM
kama baraza la katiba la kitaasisi litaipitia rasimu iliyowasilishwa
kifungu kwa kifungu na kwa kuzingatia maoni ya CCM yaliyotolewa mwanzoni
kabisa mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, wanachama wetu watashiriki
kutoa maoni yao.
Pamoja
na kazi nzuri ya Tume ya Mabadiliko ya katiba, Kamati Kuu inaiomba Tume
hiyo kueleza vizuri mchakato mzima kutoka rasimu ya kwanza mpaka rasimu
ya mwisho ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya mchakato mzima
hasa baada ya rasimu ya kwanza kutoka.
Kamati
Kuu inawasihi Watanzania kushiriki tena kwenye kutoa maoni kupitia
mabaraza ya katiba kwa rasimu ya kwanza, bunge maalum la katiba kwa
rasimu ya pili na kupitia kura ya maoni kwa rasimu ya tatu, kwa
amani,utulivu na kuvumiliana ili mwisho wa siku tupate Katiba nzuri ya
nchi yetu kwa masilahi ya Watanzania walio wengi.
Nape Moses Nnauye
CCM Secretary for Ideology & Publicity.
No comments:
Post a Comment