Friday, June 14, 2013

WARATIBU WA ELIMU MBINGA NA MIKAKATI YA KUKUZA KIWANGO CHA ELIMU

Wanafunzi wakiwa katika kituo cha masomo (Kambi) katika shule ya msingi Mwanyu iliyopo kata ya Maguu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wakati huu wa likizo, ambapo Wadau mbalimbali wa elimu wamefurahishwa na mfumo huo ambapo wanasema mfumo huu kwa kiasi kikubwa utasaidia kukuza kiwango cha elimu wilayani humo.                                  (Picha na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WARATIBU elimu kata wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma, kwa pamoja wameadhimia kuunganisha nguvu zao kwa pamoja ili kumaliza tatizo kubwa la kushuka kwa kiwango cha taaluma katika wilaya hizo, ikiwemo kuwafundisha kwa bidii watoto wanaotarajia kuanza mitihani ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari, ili waweze kufanya vyema katika mitihani yao.

Aidha wamepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na afisa elimu ya msingi wa wilaya ya Mbinga Mathias Mkali,  ambaye amekuwa akijituma katika kuhakikisha kwamba walimu wanapata mahitaji yao ya    ya shule ikiwemo vifaa vya kutosha vya kufundishia.

Kufuatia jitihada hizo zinazoendelezwa na ofisa elimu huyo hivi sasa walimu na watoto mashuleni, wamekuwa wakijituma na kufanya vizuri  hali iliyoitoa wilaya hiyo kutoka nafasi ya tano hadi kufikia nafasi tatu  kimkoa, ikilinganishwa na matokeo ya miaka mitatu iliyopita kabla ya kufika kwake akitokea wilaya ya Tunduru ambapo wilaya hiyo ilikuwa ikishika mkia.


Waratibu hao wamefikia maamuzi  hayo katika kikao maalum kilichofanyika hivi karibuni, kwenye ukumbi wa jimbo la Mbinga uliopo mjini hapa kikilenga kutafuta njia mbadala za kuongeza kiwango cha taaluma wilayani Mbinga.

Sambamba na hayo waratibu hao wamewataka watumishi wengine wa halmashauri ya wilaya hiyo kutobeza juhudi  hizo zinazofanywa sasa na ofisa elimu huyo, badala yake wamuunge mkono na sio kumvunja moyo wa kufanya kazi.

Mmoja wa waratibu elimu kata Cosmas Ndunguru wa kata ya Mbinga mjini alisema hali ya elimu katika wilaya ya Mbinga na Nyasa sio ya kuridhisha, hivyo zinahitajika nguvu za pamoja katika kuibadili hali hiyo.

Alisema aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Shaibu Nnunduma, naye amechangia kwa kiasi kikubwa kushusha maendeleo ya elimu ya wilaya hiyo, kutokana na kuendeleza chuki  na malumbano dhidi ya afisa elimu huyo wa shule za msingi huku akisema hawataki kuona mambo hayo yakiendelea.  

"Huyu Mkurugenzi ni tatizo kila mkuu wa idara anayeletwa katika halmashauri ya Mbinga, yeye anamkataa sasa sijui mwenzetu ana agenda gani ya siri, tumemvumilia vya kutosha na sasa tumefika mahali tumechoka tungemuondoa hata kwa nguvu  lakini tunaishukuru serikali imemuhamisha vinginevyo moto angeuona", alisema.

Naye Mwalimu Samwel Maridadi  mratibu elimu kata ya Rwanda amewataka viongozi wa wilaya hiyo, kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima  ikiwemo waache kujenga makundi na kupiga majungu, ambayo yanarudisha nyuma maendeleo ya wilaya hiyo.

No comments: