Hii ni ofisi ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa nje mlango na madirisha nayo yalichomwa moto kama inavyoonesha katika picha. |
Hili ni eneo la ndani ya ofisi ya Katibu wa chama cha Mapinduzi(CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo mapazia yaliyowekwa dirishani nayo yaliungua kwa moto. |
Baadhi ya Madiwani wakiwa nje ya ukumbi wa CCM, wakitafakari juu ya tukio hilo la kuchomwa moto kwa ofisi ya Katibu wao.(Picha zote na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida ofisi ya Katibu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imenusurika kuteketea kwa moto
kufuatia watu wasiojulikana, kuichoma moto kwa kutumia mafuta aina ya petroli.
Ofisi hiyo imechomwa madirisha na mlango mmoja huku ndani
yake mapazia yaliyowekwa madirishani, yakiwa yameteketea kwa moto.
Akizungumza na Waandishi wa habari Katibu wa CCM wa wilaya ya
Mbinga Anastasia Amasi alisema, tukio hilo la kuchomwa kwa ofisi yake limetokea
usiku wa Juni 20 mwaka huu kuamkia leo.
Amasi alisema kuwa yeye akiwa nyumbani kwake alipata taarifa
za kuchomwa moto kwa ofisi hiyo majira ya saa 2:07 asubuhi ya leo, ambapo
alipofika katika eneo la tukio aliona uharibifu huo uliofanyika.
Alisema baada ya kuona hali hiyo, alitoa taarifa katika kituo
kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga, na kwamba polisi walifika katika eneo la
tukio na kuchukua maelezo ya awali kwa ajili ya kuyafanyia uchunguzi.
“Nilikwenda kuripoti polisi walikuja hapa na kuchukua
maelezo, lakini tulikuta mafuta aina ya petroli lita moja ambayo yalibaki
wakati hao wahalifu wakichoma moto, hivyo nina hakika ofisi yangu imechomwa
moto kwa mafuta ya aina hiyo”, alisema Amasi.
Hali ya kisiasa wilayani humo hivi sasa si shwari, kutokana
na vuguvugu la uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga ambao ulitarajiwa kufanyika leo, lakini kutokana na hali hiyo chaguzi
hizo zimeahirishwa hadi ratiba kamili itakapotolewa tena.
Kauli ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo imetolewa katika ukumbi
wa Chama Cha Mapinduzi na Katibu huyo akiwa na Mwenyekiti wake Christantus
Mbunda, mbele ya madiwani ambao
walikusanyika kwa lengo la kufanya mkutano wa chama, na kupiga kura ya kuchagua wenyeviti wa kuwaongoza.
Pamoja na uchaguzi huo kuahirishwa, hakuna maelezo yaliyotolewa kwamba ni lini utafanyika, hivyo wajumbe waliokuwepo kwenye ukumbi huo waliambiwa watapewa taarifa kamili hapo baadaye.
Lakini baada ya muda kidogo kupita wilaya ya Nyasa iliendelea kufanya uchaguzi, ambao unafanyika katika ukumbi mdogo wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga na matokeo ya nani ameshinda, ndugu wasomaji tutaendelea kuwajuza hapo baadaye.
Pamoja na uchaguzi huo kuahirishwa, hakuna maelezo yaliyotolewa kwamba ni lini utafanyika, hivyo wajumbe waliokuwepo kwenye ukumbi huo waliambiwa watapewa taarifa kamili hapo baadaye.
Lakini baada ya muda kidogo kupita wilaya ya Nyasa iliendelea kufanya uchaguzi, ambao unafanyika katika ukumbi mdogo wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga na matokeo ya nani ameshinda, ndugu wasomaji tutaendelea kuwajuza hapo baadaye.
Tumezungumza kwa nyakati tofauti na madiwani hao ambao
hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walisema matukio hayo yanasababishwa na
viongozi wenyewe wa ngazi ya wilaya na mkoa hivyo ni vyema wakajirekebisha,
hizi ni zama za uwazi na ukweli na hawataki kulazimishwa kumchagua mtu
wanayemtaka wao.
Pia walihusisha tukio hilo la kuchomwa moto kwa ofisi ya
katibu huyo huenda linatokana na vuguvugu hilo la uchaguzi, ambalo linaonekana
mwiba kwa baadhi ya vigogo.
Hata hivyo kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Deusdedith
Nsimeki alipotafutwa ili aweze kuzungumzia juu ya tukio hilo la kuchomwa moto
kwa ofisi ya Katibu huyo wa CCM wilayani humo, hakuweza kupatikana na simu yake
muda mrefu ilikuwa imefungwa. ( Ndugu Wasomaji wa mtandao huu, tutaendelea kuwajuza nini kinachoendelea juu ya tukio hili, endelea kufuatilia mkasa huu kupitia mtandao huu )
No comments:
Post a Comment